NA ASHURA SLIM, CHUO KIKUU HURIA

MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa huduma ya maji ili kusaidia upatikanaji wa huduma   bora katika maeneo yao.

Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Msikiti Mabuluu, Mkurugenzi wa biashara na huduma kwa wateja, Kazija Mussa Msheba, alieleza hayo kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya ulipaji wa maji na huduma za mamlaka hiyo kwa ujumla.

Alisema, Serikali haina lengo la kumkomoa mwananchi bali hatua hiyo inakusudia kuimarisha huduma na maisha yao kutokana na ongezeko la watu na kupelekea kuongezeka kwa matumizi siku hadi siku.

“Idara yangu ina kazi ya kusimamia wateja, kusikiliza malalamiko yao na kuyatatua kwa wakati husika pamoja lakini pia kukusanya mapato, hivyo nawaomba wananchi waendelee kuchangia huduma ili kuimarisha uwezo wetu wa kuwahudumia,” alieleza Kazija.

Alifahamisha kuwa kiasi wanachochangia wananchi ni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji ili huduma iwe endelevu na uhakika kwa maeneo yote.

Alisema kuwa kuna mfumo maalum wa malipo unaotambuliwa kama ‘Smart Billing Manager’ (SBM) kwa ajili ya usajili wa wateja wanaolipia huduma hiyo, hivyo ni rahisi kuwatambua wanaokwepa kulipia hali ya kuwa wanapata huduma ipasavyo.

Aliongeza kuwa ulipaji wa maji unawalenga wananchi wanaopata huduma hiyo lakini pia kwa wanaokosa wanatakiwa kuripoti katika ofisi zao za wilaya au makao makuu ya mamlaka hiyo ili hatua zichukuliwe.

Aidha Kazija alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kutoka kwa wananchi ni pamoja na wizi wa maji kwa kuunga bila kufuata sheria za ZAWA, baadhi ya watu kuharibu kwa makusudi miundombinu ya maji, pamoja na kuwepo kwa mafundi vishoka.

Alifafanua kwamba mtu yeyote atakaegundulika amekiuka sheria na taratibu kwa kujiungia maji, atatozwa faini ya shilingi 500,000 au kifungo cha miezi sita hivyo aliwataka wananchi wenye tabia hizo kuacha mara moja.

Aliongeza kuwa kwa sasa wamejipanga kuhakikisha kero ya maji inamalizika kwani kupitia mradi unaotekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka benki ya EXIM kutoka India ambao una lenga la kuimarisha miundombinu hasa kwa maeneo yanayokosa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na Mwera, maeneo ya wilaya ya Kati na Fumba ambapo aliwashukuru wananchi wanaowajibika kulipia huduma hiyo kwa wakati.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kuzidisha mashirikiano na mamlaka hiyo kwa maendeleo ya taifa lakini pia kuachana na kasumba kwamba maji yanatoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo kufuata sheria pindi wanapotaka kuchimba visima binafsi ili kuepuka kupata maji yasiyo salama.