NA MADINA ISSA

WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar imepokea msaada wa dozi 100,000 ya chanjo za Covid 19 aina ya SINOVAC kutoka serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika uwanja wa Ndege wa kimataifa Abeid Amani Karume (AAKIA) na kupokelewa na Kaimu Waziri wa Afya, Omar Said Shaabani na Balozi mdogo wa China nchini, Zhang Zhisheng.

Akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya kupokea chanjo hizo, Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Omar Said Shaaban, alisema, chanjo hizo ni mwendelezo wa kupambana na ugonjwa wa Corona Zanzibar.

Alisema utaratibu wa kuanza kuzisambaza chanjo hizo ambazo zimekuwa na lengo la kuwafikia wahudumu katika sekta ya afya, watu wa maeneo ya viwanja vya ndege na wananchi wanaotembeza watalii wanaoingia nchini.

Aidha alisema chanjo hiyo ni ziada ya chanjo zilizopokelewa awali ambazo kipindi cha kwanza zilikuwa dozi 10,000 zililenga hasa kuwasaidia wananchi waliotarajia kwenda hija.

Hivyo, alisema kuwa chanjo hiyo itakwenda kuwalenga wahudumu katika sekta ya afya, watu wa maeneo ya viwanja vya ndege pamoja na wahudumu wa utalii.

Sambamba na hayo, Waziri Shaaban, alisema, serikali kupitia wizara ya afya imeshukuru uongozi wa Jamuhuri ya watu wa China kwa msaada huo na kuwataka wananchi kuondosha dhana potofu kwa chanjo hiyo ambayo dhamira yake ni kuweza kupambana na ugonjwa huo.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, itaendelea kutafuta wadau wengine ili kuhakikisha kila Mzanzibari mwenye kutaka kuchanjwa apate chanjo ili awe salama katika kupambana na ugonjwa huo wa Corona.

Hivyo, aliwataka wananchi wa Zanzibar watakaopenda kuchanja kwa hiari yao kutumia fursa hiyo ya kujikinga na covid 19 kwa kuchanja pamoja na kuchukua tahadhari zinazotolewa na wizara ya Afya katika kujikinga na maradhi hayo.

Nae, Balozi Mdogo wa China Shang Shisceng, alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar kama njia moja wapo ya kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi mbili hizo.