NA MWANAJUMA MMANGA
WAJUMBE wa Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii ya Baraza la Wawakilishi imeshauri Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) kuongeza kasi katika ukaguzi wa bidhaa hasa zinazotoka nje ili kuepuka nchi kuwa jaa la kutupia bidhaa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Yussuf Hassan Iddi aliyasema hayo wakati walipofanya ziara ya kutembelea taasisi hiyo huko Amani mjini Unguja.
Alisema kutokufanya hivyo kunaweza kuathiri hali ya biashara hasa ukizingatia kuwa dunia imeelekea zaidi katika ushindani wa kibiashara.
Alisema kumekuwa na ubabaishaji katika uingizaji wa bidhaa unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wakiwa na lengo la kujipatia fedha pasipo kujali afya za watumishi hivyo umakini wao utafanya nchi kuwa salama dhidi ya bidhaa hizo.
“Zinapoingia bidhaa ambazo hazina ubora na ni mbovu zinaathili sana na kusababisha athari za mlaji ukizingatia hasa zile za makopo, na zile zilizofungashiwa sambamba na zile za majimaji hupelekea maradhi ya kensa,” alisema Mwenyekiti huyo.
Hivyo aliiomba ZBS kuhakikisha wanafuatilia maeneo yanayopitishwa bidhaa hizo ikiwemo bandarini, viwanja vya ndege pamoja na maeneo ya kuhifadhia vyakula ama bidhaa katika maghala ili kulinda usalama ya mlaji.
Aidha walishauri umuhimu wa kuimarisha ofisi za taasisi ya zbs katika kisiwa cha Pemba ili kuweza kufanya kazi zake ikiwemo upimaji bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa kisiwa hicho badala ya kulazimika kuleta unguja.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya ZBS, Mohammed Mwalim Simai, alisema wametengeneza utaratibu wa kuwapatia elimu ya uzalishaji wajasiriamali ili kuzalisha bidhaa zenye viwango na kuwapatia alama ya ubora kwa bidhaa wanazozalisha kwa kuwafanyia unafuu wa bei.
Alisema taasisi hiyo inakabiliwa na tatizo la wazalishaji kutokuwa na vigezo vya kufikia ubora wa bidhaa zao wanazozalisha kutokana na uwezo mdogo wa wazalishaji uliosababishwa na kutokuwa na soko la kuuza bidhaa hizo kwa kukosa sifa ikiwemo za ukosefu wa vifungashio.
Kamati hiyo ya Biashara, Kilimo na Utalii pia ilipata fursa ya kutembelea maabara za kupima viwango vya bidhaa za umeme na chakula huko Amani pamoja na jengo linalotarajiwa kuwa la ofisi za taasisi hiyo baada ya kukamilika huko Maruhubi.