NA SABRA MAKAME,SCCM

MENEJA Uhusiano Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Ali Mohamed Ali, amewahimiza wauzaji wa karafuu kukubali matokeo ya ulipwaji kwa njia ya elektroniki, ili kueka usalama kwa malipo yao.

Aliyasema hayo wakati akiwa ofisini kwake Maisara kutokana na baadhi ya wananchi wakidai kuanzishwa kwa mfumo huo ni chanzo cha kupata hasara kwa wauzaji wa karafuu.

Alisema shirika limeanza kutumia mfumo mpya wa malipo kwa wakulima, watalipwa kwa njia ya simu  kwa kutumia ezypesa au benki.

Ali alieleza kuwepo kwa mfumo huo ni wazo la serikali, ili kuondosha wananchi kulipwa pesa kamili mkononi, jambo ambalo lihatarisha usalama kwa wauzaji.

Aidha, alisema kumekuwa na umuhimu wa kuanzisha mfumo huo ni kutokana na wauzaji kukabidhiwa kiwango kikubwa cha fedha mkononi, jambo ambalo hupekea baadhi kuibiwa au kutapeliwa kwa namna moja ama nyengine.

Alieleza mfumo huo utaokoa muda kutokana na hapo awali ilikua wananchi wengi wanapoteza muda mrefu kukaa kituoni kusubiria fedha hizo.

Meneja alisema kumekua na baadhi ya wananchi kutokuridhika na mfumo huo, lakini kila siku zinavyozidi kwenda wananchi wamekua wakifaidika na mfumo huo.

“Tumefanya uchunguzi tumegundua  wakulima wengi wameanza kutumia  mfumo huo tofauti na hatua ya mwanzo watu wengi walilipinga suala hilo lakini kila siku zinazokwenda wanaelewa zaidi”alisema Meneja

Vile vile, alisema kumekua na changamoto kwa baadhi ya wauzaji wa karafuu kutumia namba ambazo sio zao ,hili huwakwamisha shirika hilo kuelewa nani muhusika wa bidhaa, hizo.

Ali alisema jukumu la  kuuza karafuu ni shirika pekee lililopewa mamlaka ya kuuza,kwa yeyote ambae atauza karafuu bila ya kufata utaratibu sheria itachukua nafasi yake.