NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi, Rahma Kassim Ali, amesema kumalizika kwa ujenzi wa barabara, ukuta na bustani katika eneo la nje ya jengo jipya la abiria (Taminal III) kutachochea ongezeko la ajira kwa vijana nchini.

Alieleza hayo hivi karibuni mara baada ya kukagua ujenzi wa maeneo hayo ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alipofanya ziara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, mapema mwaka huu.

Aidha alieleza kuwa ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ambapo kwa kiasi kikubwa maagizo hayo yametekelezwa vyema na kwamba hautokawia kumalizika.

Rahma alifahamisha kuwa watakapomaliza ujenzi huo, vijana watapata ajira kupitia kampuni binafsi na taasisi za serikali zitakazokuwa zinatoa huduma uwanjani hapo na kupunguza idadi ya vijana wasiokuwa na ajira.

“Maendeleo ya ujenzi huo umefikia hatua nzuri na utakapomaliza wataweza kuajiri kampuni ya kusimamia usafi ambapo itaweza kuongeza pato la nchi na kupunguza idadi ya vijana wasiokuwa na ajira,” alisema.

Naye Meneja wa mradi wa uwanja huo, Khamis Omar Shemey, alisema kwa upande wa barabara imeshakamilika kinachosubiriwa ni uwekaji wa taa ili iweze kuleta sura nzuri katika eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu ukuta, Khamis, alisema wizara imefanya mchakato wa kumtafuta mkandarasi na kwamba kampuni ya CRG imeanza kujenga ukuta huo ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50.

“Ukuta unajengwa kiwandani na hapa unakuja kubandikwa tu na kinachotegemewa ni kuja kuwekwa wakati utakapomalizika huko kiwandani” alisema.