BLOEMFONTEIN, AFRIKA KUSINI

MAMLAKA za Afya nchini Afrika Kusini zimewahimiza wanawake wajawazito na wenye nia ya kuzaa wapate chanjo ya UVIKO-19.

Ushauri huo ulitolewa na Kamati ya Ushauri ya Mawaziri (MAC) kuhusu chanjo za UVIKO-19 na ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia na kutathmini usalama na utendaji kazi wa chanjo hizo.

Ushauri uliotolewa na kamati hiyo ya mawaziri ulisema ingawa wasiwasi ni mdogo, lakini wanawake wajawazito na waliopanga kupata watoto wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na ugonjwa wa corona ikilinganishwa na wanawake wengine.

Ushauri huo wa kimaandishi ulisainiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo, Dk Nicholas Crisp ambaye alisema kuwa, ana matumaini wanawake wajawazito na wenye nia ya kuzaa wako katika mazingira ya kupata zaidi UVIKO-19.

Siku chache zilizopita, ripoti zilisema kuwa, idadi ya kesi za ugonjwa wa corona zilizothibitishwa barani Afrika ilikuwa imepindukia milioni saba na laki saba.

Kwa mujibu wa ripoti ya Africa CDC, nchi zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa UVIKO-19 barani humo ni Afrika Kusini, Morocco,Tunisia na Ethiopia.

Kwa sasa ni asilimia 2.4 tu ya watu wa Afrika waliopata chanjo za COVID-19 huku kukiwa na mkakati wa kuhakikisha kuwa idadi hiyo inaongezeka hadi asilimia kumi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.