NAIROBI, KENYA

JUKWAA la Utalii la Afrika Mashariki (EATP) lilizitaka Tanzania, Burundi na Sudan Kusini kujiunga na utaratibu wa viza ya pamoja ya utalii katika Afrika Mashariki.

Akizungumza baada ya Baraza la Biashara la Afrika Mashariki na EATP kusaini Makubaliano ya Maelewano yanayolenga kutangaza Jumuiya ya Afrika Mashariki kama kituo kimoja cha utalii, Frank Mugisha, mkurugenzi mkuu wa EATP alisema Kenya, Uganda na Rwanda tayari wameshajiunga na utaratibu wa kutoa viza ya pamoja ya utalii wa kikanda.

Mugisha alisema tangu kutokea kwa mripuko wa janga la UVIKO-19, mapato ya sekta ya utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC yamepungua sana.

Hivyo janga hili limezifunza nchi wanachama kushirikana na kuunganisha nguvu pamoja kwenye sekta ya utalii ili kujiinua kwenye vivutio mbalimbali vya utalii.

Kwa mujibu wa EATP viza ya pamoja italeta mauzo mengi ya vifurushi vya utalii kwa watalii wa nje kwa kutumia vizuri maeneo ya utalii yaliyokaribu kijiografia ya EAC.