MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amedai hakuvunjika moyo na klabu baada ya kumkosa, mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Kylian Mbappe wakati wa usajili wa majira ya joto.
‘Blancos’ walielekeza mawazo yao kwa mshambuliaji huyo aliyetwaa Kombe la Dunia na Ufarabsa baada ya kumuona akiingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake huko Paris Saint-Germain.
Ofa ya euro milioni 220 kwa yoso huyo mwenye umri wa miaka 22 iliwasilishwa kabla ya tarehe ya mwisho kupita, lakini, PSG ilikataa kuidhinisha uuzaji wa fedha kubwa wakati wakishikilia matumaini kwamba ni hazina inayostahili kubakishwa kwa ajili ya kumpa mkataba mpya.
Huku Madrid ikiripotiwa kuwa inataka kumchukua Mbappe kama mchezaji huru mnamo 2022, Ancelotti aliwaambia waandishi wa habari: “Hatujavunjika moyo, lakini, ni wazi kuwa yeye ni mchezaji mzuri na tunamtakia bahati njema. Tuna kikosi chenye nguvu”.
Miamba hiyo tayari ina mchezaji mmoja wa kimataifa wa Ufaransa kwenye vitabu vyao kama Karim Benzema, wakati Gareth Bale amewasha cheche zake tangu aliporudi Hispania kutoka mkopo wa msimu mmoja huko Tottenham.
Ancelotti alimleta nyota huyo Wales wakati alipokuwa akifundisha na haishangazi kuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 akistawi tena.
Alisema kuhusu Bale: “Ameanza vizuri na lazima aendelee. Nadhani bado anaweza kuimarika na kuwa katika kiwango bora. Lazima nionane na wale wote ambao wamecheza na timu zao za taifa.”
Wakati Madrid wakishindwa kumtwaa Mbappe kwenye dirisha la siku ya mwisho, walifanya mikataba kamili kwa David Alaba na Eduardo Camavinga.
Camavinga anahesabiwa kuwa mojawapo ya matarajio moto zaidi ya mpira wa miguu huko Ulaya huku kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18 akitupia macho huko Rennes.
Yoso huyo jana alitarajiwa kucheza dhidi ya Celta Vigo, lakini, Ancelotti hatokuwa akikimbilia ukuaji wa kijana huyo.
Mitaliano huyo aliongeza juu ya Camavinga: “Yuko sawa, anafurahia na amehamasika kuwa hapa. Anafanya mazoezi vizuri kwenye kikosi na kwa kweli anaweza kuwepo kwenye mchezo wa leo (jana).
Mwenyekiti wa Paris Saint-Germain, Nasser al-Khelaifi, amewahi kunukuliwa akisema, Mbappe, hana sababu ya kuiacha klabu hiyo baada ya kuwasili kwa Lionel Messi, ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili.
“Kylian ni mkazi wa Paris, ni mshindani. Alisema alitaka timu yenye ushindani,” alisema Al-Khelaifi.
“Kwa sasa hakuna aliye na ushindani zaidi yetu. Hana sababu ya kufanya lolote jengine, zaidi ya kubakia”.
Mwezi Mei, mshambuliaji aliiambia Canal Plus kuwa anataka kuwa sehemu ambako anaweza hasa kushinda ambako kuna mpango mzito.”
Mbappe bado hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Parc des Princes, tofauti na Neymar, ambaye hivi karibuni alikubaliana mkataba ambao utambakiza PSG hadi mwaka 2025.
Mshambuliaji huyo Mfaransa anatarajiwa kuungana na Neymar na Messi katika safu ya ushambuliaji ya PSG.(AFP).