NA TATU MAKAME

UGONJWA wa corona ni miongoni mwa magonjwa yaliochukua nafasi kubwa duniani na kupata umaarufu kuliko mengine.

Ugonjwa huo unatokana na virusi vya Corona COVID-19 ambao ni mripuko mpya uliogunduliwa mwaka 2019 ambao haukuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa binaadamu.

Ugonjwa huo ulianza nchini China kutokana na kujitokeza kwa virusi vilivyosababishwa na virusi vya Corona (Covid 19) ambao huanza kwa mafua ya kawaida hadi magonjwa makali kama vile matatizo ya kupumua (MERS-CoV) na SARS-CoV.

Hata hivyo kujitokeza kwa ugonjwa huo hapa nchini wananchi walikuwa na hofu kubwa ya kupata hofu ya kupata maambukizi kutokana na upya wa maradhi hayo.

Aidha baada ya kujitokeza kwa ugonjwa huo serikali na taasisi mbalimbali binafsi zilijitokeza kutoa elimu juu ya namna ya kuwataka wananchi kujikinga na ugonjwa huo sambamba na kuwatoa hofu juu ya maambukizi ya virusi hivyo.

Hata hivyo mbali na elimu pia taasisi hizo zilishiriki kutoa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo ikiwemo masokoni kwa kutoa vitakasa mikono (sanitaiza) kwenye daladala kubandikwa vipeperushi ambavyo vinawataka wananchi kujikinga na maambukizi hayo ya virusi vya corona.

Mwandishi wa Makala haya alifuatilia kujua ni kwa kiasi gani taasisi binafsi zilijitokeza kutoa misaada ya kujikinga na corona sambamba na na kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu kuepusha maambukizi na kuwatoa hofu wananchi kujikinga na maambukizi hayo.

WANANCHI WANASEMAJE KUHUSU KUPATIWA MSAADA NA TAASISI ZISIZO ZA RERIKALI.

Wakizungumza na mwandishi wa Makala haya wananchi katika maeneo mbalimbli ya Zanzibar walisema kuwepo kwa taasisi zisizo za serikali zimesaidia kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo hapa nchini.

Walisema awali walikuwa na hofu juu ya kujitokeza kwa ugonjwa huo na jinsi unavyoambukiza hasa katika mikusanyiko ya watu.

Fdhil Hilali Ame alisema elimu inayotolewa na asasi za za kiraia Zanzibar (ANGOZA) ilipunguza hofu ya kusambaa kwa ugonjwa huo kwa wananchi.

Alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujiepusha na mikusanyiko ambayo isiyo ya lazima ambayo inaweza kusababisha maambukizi kwa kiasi kikubwa kwa jamii.

“Tangu asasi za kiraia zilipoanza kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo wananchi wengi wameondokana na hofu ya kupata maambukizi na kujua namna ya kujiepusha na mikusanyiko.

Mwema Juma Saadat, alisema  kabla ya kupatiwa elimu wananchi wengi walikuwa na hofu ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo, lakini elimu iliyotolewa na taasisi hizo zilisaidia kuimarisha uthubutu wa kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema mbali na elimu inayoendelea kutolewa kwa taasisi hizo lakini pia utoaji wa vitakasa mikono kwenye mikusanyiko ni njia moj wapo iliyotumika kupunguza hofu ya ugonjwa huo ambapo wananchi wengi wamekuwa wakiitikia wito wa kuvaa barakoa.

“Licha ya serikali kutoa elimu ya kujikinga lakini utoaji wa vitakasa mikono umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza hofu ya watu kuambukizana kabla ya kuingia kwenye mikusanyiko”, alisema.

Thuwaiba Iddi Mabrouk alisema utoaji wa vitakasa mikono kwenye mikusanyiko umesaidia wananchi kuendelea kuamini kuwepo kwa taasisi hizo na kupunguza hofu juu ya kupata maambukizi.

Jela Hijja Hindi alisema njia zilizotumiwa na asasi za kiraia (ANGOZOZA) za kubandika stika kwenye daladala kuhusu tahadhari ya ugonjwa wa corona umeongeza umakini juu ya kujikinga na ugonjwa huo kwa wananchi.

“Ukiingia kwenye daladala unaona ujumbe unaoashiria kujikinga na maambukizi kwa kuwataka abiria kuchukua tahadhari,kwa kiasi kikubwa ulisaidia kuongeza tahadhari juu ya maambukizi ya ugonjwa huo”, alisema.

JUMUIYA YA VIJANA

Mwenyekiti wa Baraza la vijana Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja Hassan Ali Nassor, alikiri kupokea vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo kutoka kwa jumuiya zisizo za serikali (ANGOZA) tangu kuingia kwa ugonjwa huo.

“ANGOZA ilikuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na ugonjwa huu kwa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari lakini kubwa zaidi ni suala la kutoa vitakasa mikono.

Alisema utoaji huo wa elimu kwenye makundi ya watu na kutoa muongozo wa kujikinga na ugonjwa huo kutoka taasisi ya angoza ulisaidia kwa wananchi kujua umuhimu wa kujikinga na afya zao kwenye mikusanyiko.

JUMUIYA YA DALADALA INASEMAJE

Mratibu wa umoja wa madereva na utingo wa daladala Zanzibar, Maulid Mwinyi Khamis, alisema  alipokea vipeperushi kutoka Mwamvuli wa asasi za kiraia ANGOZA  na kuvisambaza kwa madereva ili kubandika kwenye daladala ili wananchi wanaotumia usafiri huo wapate elimu na waondokane na hofu ya kupata maambukizi.

“Wananchi wengi waliokuwa wakitumia usafiri wa daladala walikuwa na hofu lakini tuliweza kuwakinga wateja wetu kwa kuwanawisha mikono na kuwataka wavae barkoa kabla ya kupanda kwenye gari ili kuepusha maambukizi mapya”, alisema.

Alisema kutolewa kwa stika hizo kulipunguza hofu kwa wananchi kupata maambukizi wanapotumia usafiri wa daladala na kuendelea kuwa na Imani na usafiri huo.

“Tulipata kipindi hata abiria hawaji mjini wakihofia kupata maambukizi lakini kubandikwa stika hofu hiyo iliondoka kwa wananchi”, alisema.

ASASI ZA KIRAIA ZINASEMAJE

Ofisa Msaidizi wa miradi kutoka ANGOZA, Hassan Saidi Salum, alisema mafanikio hayo yalifikiwa baada ya Shirika la Internews kuandaa mradi wa pamoja ambao uliwawezesha kusambaza ujumbe kwa kutumia mtandao huo kutoa elimu kwa wananchi katika mikusanyiko ya watu kuhusu athari za ugonjwa huo kwa jamii.

Alisema mafanikio ya mradi wa boresha habari wa iternews ulitoa taaswira halisi ya mashirikiano kati ya asasi za kiraia, vyombo vya habari na serikali ambapo ushirikiano wa taasisi hizo ulisaidia kutoa elimu na vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona katika mikusanyiko ya watu.

“Baada ya kuona ugonjwa huo ni mpya na watu wengi wanahofu ya kuambukizwa tumeona bora tutoe vifaa na elimu kwa watu kwenye mikusanyiko ya watu ikiwemo masokoni na sehemu nyengine ili kuondosha hofu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo”, alisema.

Hata hivyo Ofisa miradi huyo alisema wamefanikiwa kutoa elimu na vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali kwenye mikusanyiko.

“Hata kwenye madaladala tulibandika stika na tukaondosha hofu kwa wananchi juu ya kupata maambukizi na wakawa na imani ya kutumia usafiri huo”, alisema.

Hata hivyo alizitaka taasisi nyengine kujitokeza kutoa misaada ikiwemo vitakasa mikono ili kila mwananchi anaekwenda sehemu za mikusanyiko kunawa mikono ili kulinda usalama wa afya yake.

VIPI UTAJIKINGA NA CORONA

Miongoni mwa njia za kujinga na ugonjwa huo ni kunawa mikono kila mara na kuepuka kugusa uso wako kwa mikono ili kuepuka kupata maambukizi.

Kujenga tabia ya kukaa umbali wa mita 2 au futi 6 mbali na wengine na kukaa nyumbani ikiwa mtu hana dharura maalum.

Wataalamu wa afya wanashauri mtu atakaekwenda chafya au kukohoa kuweka mkono au kujiziba kwa kitamba kwa kutumia visugudi na sio viganja vya mikono.

Aidha kuonana na daktari kwa mjamzito kuangaliwa afya zao na kuwakinga watoto na maambukizi mara tu wazaliwapo.

Wataalamu wa afya wamekuwa wakihimiza wananchi kuona umuhimu wa kujikinga hasa pale wanapokwenda kliniki kwa mama wajawazito.