NA KHAMISUU ABDALLAH
KITENGO cha kupambana na dawa za kulevya, kimemtia mbaroni kijana Ali Azidu Kaliali mwenye umri wa miaka 20 mkaazi wa Kisauni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mara baada ya kutiwa mbaroni, kijana huyo alifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.
Alifikishwa mbele ya Hakimu Nazrat Suleiman na kusomewa shitaka la kupatikana na dawa za kulevya na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Said Ali.
Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa, Juni 3 mwaka huu majira ya saa 6: 40 za asubuhi huko Kisauni Muharitani, bila ya halalai alipatikana na mfuko wa karatasi rangi ya kaki ndani yake mkiwa na nyongo 22 za majani makavu yenye uzito wa 36.9318 gramu, yanayotuhumiwa dawa za kulevya aina ya bangi, kitendo ambacho ni kosa kisheria
Alidai kutenda hiyo ni kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 24 (a) cha sheria namba 1 ya mwaka 2019 sheria za Zanzibar.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.
Kuhusu ombi la dhamana, Mwendesha Mashitaka huyo alidai hana pingamizi ikiwa mshitakiwa atawasilisha wadhamini madhubuti na kuhudhuria mahakamani kila anapo hitajika.
Hakimu Nazrat, alikubaliana na maombi ya pande zote mbili na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9 mwaka huu, huku akiuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
Mahakama pia ilimpatia masharti ya dhamana mshitakiwa na kufahamisha kuwa, endapo akishindwa kuyatekeleza atakwenda rumande.