NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imezindua mpango wa kulipia tiketi kidogo kidogo – Kibubu kwa wananchi na wateja kuweza kusafiri kutumia ndege hizo ndani na nje ya nchi.

Uzinduzi huo umefanyika jana, jijini hapa, ATCL imewajumuisha wananchi na wadau wote kununua tiketi za safari za ndege kupitia mpango wa Kibubu, ambao unalipia kwa awamu mpaka pesa zikikamilika ndio unakabidhiwa tiketi yako.

Akizungumza na wandishi wa Habari, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Jaephat Kagirwa amesema mpango huo utawahusu walengwa kulipia tiketi zao kidogo kidogo na awamu ya mwisho kukamilika malipo mteja atapewa tiketi yake.

Alisema ununuzi wa tiketi kwa kutumia Kibubu, ambapo kwa sasa watalipia fedha moja kwa moja katika kampuni hiyo, na hapo baadae watakutana na mabenki ili kuweza kulipia huko na kianzia cha kwanza ni shilingi 50,000 kwa mteja atayeweka booking ya tiketi ya kusafiri ndani na nje mpaka China safari zitakapoanza.

“Mpango huu unatarajia kuleta unafuu katika kulipia gharama za usafiri wa ndege, pia kuongeza idadi ya abiria watakaotumia huduma zetu ambao awali hawakuwa na fursa hiyo kabla ya mpango huu”, alisema.

Naye Meneja wa Mtandao wa Safari na Msimamizi na Mapato, Edward Nkwabo alisema abiria atatakiwa kufanya maandalizi ya safari (booking) yake kwa ajili ya kusafiri kisha atalipa kwa awamu ya kwanza kwa pesa taslimu katika Ofisi zao za ATCL, ambapo mteja atapewa tiketi yake baada ya kukamilisha malipo yote na nauli ya safari husika.

Aidha alifafanua kuwa, watatekeleza mpango huo pamoja kwa kupokea malipo kupitia benki mbali mbali na Taasisi nyengine za fedha, ambapo mteja ataingia nazo mkataba.

Alisema njia nyengine ya kurahisisha utekelezaji wa mpango huo utakuwa ni kufanya malipo kupitia mitandao ya simu, baada ya kampuni ya Ndege ya Tanzania kuingia mkataba na mitandao ya simu na mifumo yote ya malipo ikishakukubalika.