NA ABOUD MAHMOUD
HATIMAE kilio cha siku nyingi kwa wadau, mashabiki pamoja na timu za soka, ambazo zinashiriki ligi kuu visiwani sasa hivi kimemalizika.
Katika msimu huu wa ligi kuu ya visiwani humu tumeshuhudia benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kubeba jukumu la kuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo.
Udhamini huo ambao unakadirikiwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 340 kwa msimu wa mwaka 2021-2022, ambapo utashirikisha timu 16 zinazoshiriki ligi kuu hiyo.
Lakini mbali na udhamini huo wa PBZ kampuni mbali mbali zilijitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya kuendeleza ligi kuu ya Zanzibar .
Miongoni mwa kampuni ambazo zimejitokeza na kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia ligi hiyo ni pamoja na GSM,Azam Media, Shirika la Bima la Zanzibar pamoja na kampuni ya Z-MUX Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zimethibitisha kwamba jumla ya shilingi milioni 940,510,000 zilikusanywa katika harambee maalum, iliyoendeshwa hivi karibuni katika ukumbi wa Madinat Bahr na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah.
Hili ni jambo jema na faraja kwa wananchi na wapenda soka visiwani humu kwani ligi kuu ya Zanzibar imekosa udhamini kwa kipindi kirefu hivi sasa.
Baada ya kuondoka kwa udhamini wa kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt mkataba wa miaka mitatu wa shilingi milioni 140, ambao walikua wadhamini na kuondoka kwa kampuni ya simu ya mkononi ya Zantel.
Kwa hakika ni jambo la furaha na la kupongezwa kwa Serikali ya awamu ya nane chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa jitihada ilozichukua katika kuhakikisha ligi ya msimu huu inapata udhamini.
Imani yangu kubwa kuwepo kwa udhamini katika ligi kuu ya Zanzibar, kutasaidia kurejesha hadhi ya mchezo huo kama ilivyokua miaka ya nyuma.Lakini mbali na udhamini wa ligi kuu pia kumejitokeza mtu mwengine ambae anajulikana kwa jina la Alex Morfaw kutoka nchini Ufaransa, ambae amedhamiria kuwekeza katika kudhamini ligi ya vijana .
Morfaw katika mazungumzo yake alisema kwamba ataendelea kushirikiana na Zanzibar, kuimarisha na kukuza michezo ili kuinua kiwango cha mpira wa miguu.
Kwa hakika hili ni jambo jema kwani hichi nacho kilikua kilio kikubwa na cha siku nyingi kwa vijana wetu, ambao wamekua mstari wa mbele kujikita kwenye soka bila ya kupata wadhamini.
Tukitembelea viwanja vingi vya soka hapa nchini utakutana na watoto wengi ambao wamejikusanya na kuanzisha timu zenye lengo la kukuza mchezo huo lakini ukiwauliza kilio chao ni kucheza soka bila ya mafanikio yoyote.
Hivyo basi ujio wa Morfaw hapa nchini utaweza kuinua soka la vijana wetu ambapo watacheza kwa furaha na mafanikio makubwa hapo baadae, kwani tutakua na vipaji vingi na kuuzwa kwa mataifa mengine.Lengo langu ni kuiomba Serikali kuzidisha juhudi ya kutafuta wadhamini wa michezo mengine.
Katika visiwa vyetu ipo michezo mingi ambayo inahitaji kupatiwa udhamini ili iweze kufanya vizuri na kuitangaza vyema nchi yetu.Baadhi yao ni pamoja na netiboli, kikapu, mpira wa mikono na wavu ambayo nayo inahitaji kupatiwa udhamini ili iweze kufanya vizuri.
Baadhi ya michezo niliyoitaja hapo juu imekuwa na hali ngumu kiasi kwamba, hata wakitaka kushiriki katika mashindano yanayofanywa nje ya Zanzibar hushindwa kushiriki.Tumeshudia kuandaliwa mashindano mbali mbali nje ya Zanzibar na timu za michezo hiyo kushindwa kushiriki ambapo wanaoshiriki ni timu za askari na sio raia.
Hivyo ni wajibu wa kila mmoja na sio Serikali peke yake kujitahidi kutafuta wadhamini wa michezo mengine, ili Zanzibar ifanikiwe kung’ara katika ulimwengu wa michezo.