MIONGONI mwa manung’uniko makubwa katika jamii yetu ya kizanzibari ni kuporomoka kwa maadili, ambayo siku za nyuma yalitutafautisha na jamii nyengine na kuiwezesha Zanzibar kujizolea heshima kubwa.

Sehemu kubwa ya jamii kwa wakati imebakia kulalamika kutokana mabadiliko ya vijana, huku kukiwa na masuali mengi kama mbona Zanzibar hii sio ile ya zamani ambayo watu kutoka maeneo tafauti walikuja kujifunza maadili na ustaarabu wa kupigiwa mfano.

Dhana kuu iliyojengeka ni kuwa tatizo hili limekuzwa na mabadiliko makubwa ya kiulimwengu ambayo yameifanya dunia kuungana kuwa kama kijiji kutokana teknolojia kurahisika mawasiliano yaani utandawazi.

Utandawazi unalalamikiwa kuwa chanzo cha kuvurugika misingi ya heshima, kupodea kwa adabu na maadili tuliyoyarithi kwa miaka mingi kutoka kwa wazee wetu, misingi ambayo hivi sasa tunakubaliana kwamba ni kinga ya majanga mengi yanatukumba.

Si ajabu tena kumuona mwanafunzi wa skuli ya msingi akitembea na simu ya kisasa ina huduma za mtandao, hivyo kumuwezesha kuangalia atakacho, bila ya kizuizi.

Bila shaka hali hiyo imewafanya vijana na wasichana wetu, wakiwemo wanafunzi kutumia muda mwingi kwenye simu kujifunza na kujua mambo ambayo hayalingani na umri wao.

Kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, Twitter na WhatsApp huko kuna kila aina ya uchafu na utovu wa maadili na kwamba bahati mbaya sana hakuna kuzuizi cha vijana ambao wapo chini ya umria wa miaka 18 kutoona yale yanayorushwa.

Hata hivyo, kuna mazuri ya kujifunza yanapatikana huko kwenye mitando ya kijamii, lakini kwa bahati mbaya vijana wetu wengi hawajifunzi mambo mazuri badala yake wanajifunza mambo ambayo yanavunja mila silika na maadili.

Vijana na wasichana wetu katika jamii wanatumia mitando hiyo kutukanana, kukashifiana, kushambuliana na kutumiana ujumbe mbaya, jambo ambalo linadhihirisha kuharibika kwa maadili yetu.

Imefikia hatua kila mtu anaogopa kumkanya mtoto wa mwenzake, na pengine anajua kwa kufanya hivyo anaweza kukutwa na jambo linaloweza kuwa kubwa sana na kufikia hatua ya mzazi kumkingia kifua mwanawe na pengine mzee aliyejitolea kumkanya mtoto kufikia hatua ya kushitakiwa kwenye vyombo vya dola.

Pamoja na kuwepo kwa changamoto nyingi za kimalezi kama jamii lazima kama wazee tuwe na mikakati itakayohakikisha tunarejesha mila na silka zetu za zamani hali ambayo itarejesha maadili yetu.