NA ABOUD MAHMOUD

VIJANA nchini wameshauriwa kushiriki katika michezo ya aina mbali mbali, ili kufikia malengo waliojipangia na  kujiepusha na vitendo vitakavyosababisha kuleta madhara kwao na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais mstaafu, Balozi Seif Ali Iddi, wakati alipokua akifungua bonanza la michezo lililoandaliwa na Jumuiya ya Vijana wa Mwembetanga katika uwanja wa Mao Zedong.

Balozi Seif alisema ni wajibu wa vijana kushiriki katika michezo kwani inasaidia kuleta mafanikio mengi ikiwemo kupata nafasi za ajira ndani na nje ya nchi.

“Michezo ni afya,burudani na pia ni ajira nawashauri wanangu na wajukuu zangu kushiriki katika michezo, ili muweze kufikia malengo mazuri ya maisha yenu na kuitangtaza vyema nchi yetu,”alisema.

Aidha alieleza kwamba vijana wengi wa nchi za Afrika wamefanikwa kucheza soka la kulipwa katika nchi mbali mbali duniani, hivyo ipo haja vijana wa Zanzibar kujikita katika soka na kupata nafasi kama wanazopata wenzao.

Hivyo aliwataka makocha wa mchezo wa soka kuwaandaa vijana wadogo vizuri ili waweze kuwa wachezaji bora na kuleta mafanikio katika taifa.

“Nimeshuhudia hapa uwanjani kuona vipaji vya watoto wadogo wanavyocheza mpira, wito wangu kwenu makocha kuendeleza vipaji vya watoto ili baadae Zanzibar iwe na wachezaji wengi wa kulipwa,”alisema.