MADRID, Hispania
UONGOZI wa Barcelona umesitisha zoezi la kuachana na meneja wa kikosi hicho, Ronald Koeman, kwa kuhofia kumlipa fedha nyingi kama fidia za kuvunja mkataba wake.
Koeman amekua katika wakati mgumu klabuni hapo kufuatia kikosi chake kuwa na matokeo mabaya, jambo ambalo liliibua minong’ono huenda akatimuliwa kazi wakati wowote.

Miamba hiyo haiwezi kumfukuza Koeman mwenye umri wa miaka 58 bila ya kumlipa karibu pauni milioni 10 kama fidia ya kuvunja mkataba wake.
Hata hivyo, kama mambo yataendelea kuwa mabaya kwa meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, huenda akapewa muda wa mwezi mmoja, na kama atashindwa kufikia lengo, ndipo ataonyeshwa mlango wa kutokea.

Aliyewahi kuwa meneja wa klabu hiyo, Roberto Martinez anatajwa na Bodi ya Barca kuchukua nafasi ya Koeman, endapo atashindwa mtihani unaomkabili kwa sasa.
Barcelona jana ilitarajiwa kucheza mechi ya ‘La Liga’ dhidi ya Cadiz kabla ya kurejea nyumbani Nou Camp Septemba 26 kuikaribisha Levante.

Miamba hiyo itakuwa mgeni wa Benfica ifikapo Septemba 29 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuwavaa mabingwa wa Hispania, Athletico Madrid katika ‘La Liga’ hapo Oktoba 2.

Wakati huo huo, Barcelona imeripotiwa kuwa wameamua kufungua mazungumzo na nyota wao Ousmane Dembele juu ya hatma ya mkataba wake mpya na klabu hiyo.
Nyota huyo mwenye uraia wa Ufaransa bado ameshindwa kucheza mechi yeyote ya Barcelona msimu huu kwa sababu ya changamoto ya majeraha.

Mkataba wake wa sasa uko mbioni kufikia tamati majira ya joto mwakani, na nyota huyo kwa sasa yupo huru kufanya mazungumzo na klabu nyengine.

Hata hivyo, ripoti zinasema, Barca inajiandaa kuhakikisha nyota huyo haendi popote.
Tarifa zinasema kuwa klabu inapanga kufanya mazungumzo ambayo yanatarajiwa kukamilika hadi kufikia mwezi Januari.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, amecheza michezo 118 tokea alipowasili Nou Camp akitokea Borusia Dortmund mwaka 20017, akifanikiwa kuona lango mara 30 na kutoa usaidizi katika michezo kadhaa.(AFP).