LUSAKA, ZAMBIA

SHIRIKA moja la uangalizi wa matumizi ya tumbaku limedai kampuni kubwa ya tumbaku ya BAT ilizilipa nchi kumi za Afrika katika kipindi cha miaka mitano ili kushawishi sera za afya na kuhujumu washindani wake.

Katika ripoti mbili zilizotolewa jana, shirika la STOP limesema kampuni hiyo inadaiwa kulipa zaidi ya dola laki sita kama pesa taslimu, magari, na michango ya kampeni kwa wanasiasa, wabunge, wafanyakazi wa umma, waandishi wa habari na wafanyakazi katika kampuni ambazo ni washindani wake wa biashara kati ya mwaka 2008 na 2013.

Shirika la STOP linasema kampuni ya BAT ilifanya vitendo hivyo kana kwamba iko juu ya sheria ambapo iliwalenga vijana wa Afrika.

Nchi zilizotajwa katika ripoti hiyo ni Burundi, Visiwa vya Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Rwanda, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia.