NA MWAJUMA JUMA

KUTOCHEZWA kombe la Muungano kumechangia kuporomosha soka baina ya wachezaji wa Bara na Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na mdau wa michezo  Salum Bausi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika uwanja wa Amaan.

Alisema wakati michuano hiyo inafanyika wachezaji wa Zanzibar na Tanzania Bara walikuwa na uhusiano wa karibu jambo ambalo kwa sasa halipo.

Alisema yeye binafsi ameona faida kubwa ya mashindano hayo kwani anaposafiri kwenda Tanzania Bara, hupata nafasi ya kukutana na wachezaji ambao walikutana wakati wakicheza pamoja.

Hivyo alisema  ni vyema kukaandaliwa mpango madhubuti wa kuhakikisha timu za Tanzania Bara na Zanzibar, zinakutana kwa kucheza pamoja ili kurejesha mahusiano mazuri zaidi ya kimichezo baina ya wachezaji hao.

Bausi ambae pia ni mwalimu wa mpira wa miguu, alisema pamoja na kuwa inaonekana ligi hiyo kwa sasa haina umuhimu, kwani kila upande unapata uwakilishi wake kimataifa, lakini ni vizuri kukaandaliwa utaratibu wowote ambao unaonekana utaleta manufaa kwa wachezaji wao.

Alifahamisha kwamba wakati wao wanacheza kombe hilo walijisikia fahari sana na mpira wao ulizidi kukuwa, lakini hivi sasa unaonekana kufa kutokana na kukosa upinzani.

Sambamba na hayo pia alisema kwamba wachezaji wa Zanzibar wanapokutanishwa na timu za Bara wanapata fursa nzuri ya kuonekana kusajiliwa na kupata ajira.