NA KHAMISUU ABDALLAH

BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeendelea kuongezeka kwa mwezi Agosti kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama za uingizaji wa bidhaa hiyo katika bandari ya Dar es Salam.

Ofisa Uhusiano kutoka Mamlaka ya Udhitibi wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Hassan Juma Amour, akitangaza bei hizo zitakazoanza kutumika leo kwa vyombo vya habari huko ofisini kwake Maisara, alisema bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imepanda ukilinganisha na mwezi uliopita.

Aidha alisema bei ya petroli itauzwa kwa shilingi 2,461 Kwa Lita moja mwezi huu kutoka shilingi 2,379 kwa mwezi uliopita tofauti ya shilingi 82 sawa na asilimia 3.45.

Alisema mafuta ya dizeli yatauzwa kwa shilingi 2,326 kwa mwezi huu kutoka shilingi 2,287 kwa mwezi uliopita tofauti ya shilingi 39 sawa na asilimia 1.71.

Kwa mafuta ya taa alisema bei ya rejareja itakuwa shilingi 1,729 kwa mwezi huu kutoka shilingi 1,711 kwa mwezi uliopita tofauti ya shilingi 18 sawa na asilimia 1.05.

Aidha akizungumzia sababu zilizopelekea kupanda kwa bei hizo, alisema ni pamoja na kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia.

Sababu nyengine ni kuporomoka thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola za kimarekani, gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Hata hivyo, alisema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani kwa mwezi uliopita ili kupata kianzio cha kufanyika mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi huu.

Sambamba na hayo, alibainisha kuwa licha ya kuwa mafuta yameongezeka lakini yapo ya kutosha kwa matumizi ya Zanzibar, kwani hivi karibuni serikali kupitia ZURA imetiliana saini na kampuni ya GBP ya Tanzania kwa ajili ya kuleta mafuta Zanzibar na kuondosha changamoto ya upungufu wa nishati hiyo nchini.

Mbali na hayo alisisitiza kwamba ZURA haiamui kupanda na kushuka kwa bei hiyo bali inaangalia vigezo ambavyo vinafanywa kwa uwazi.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuhakikisha kuwa bei zilizotangazwa ndio bei halali na kuwasisitiza kununua mafuta katika sheli zilizokuwepo kihalali ili kuepuka kuuziwa mafuta ya magendo na kudai risiti.