- Ni Mkaazi wa Manyaga
- Alikuwa akifikisha hadi pishi 30 kwa siku
- Kilichomsukuma ni kushindana na wake wenza
- Amefanikiwa kumiliki shamba la mikarafuu na ng’ombe kwa kazi hiyo.
Na Amina Khamis, Maelezo, Pemba
“ MCHUMIA JUANI HULIA KIVULINI”.Usemi huu sio wangu bali ni wahenga waliokuwa wakikitukuza Kiswahili wenye maana ya kuwa raha haiji ila baada ya kutoka jasho. Kwa mana nyengine kuwa mafanikio hayaji ila baada ya jitihada kupita.
Zanzibar yaani Unguja na Pemba, imejaaliwa na kuwa na njia za kipekee za uchumi wake moja wapo wa njia hizo ni zao la karafuu,ambalo linachangia uchumi kwa nafasi ya pili baada ya utalii.
Pemba ambayo maarufu kwa jina la ‘Jazeratul khadhra’ kwa maana ya kisiwa cha kijani, kimejaaliwa kuwa na neema kubwa ya zao la karafuu kuliko Unguja ambako nazi ndio ilikuwa zao kubwa zaidi .
Hali hiyo iliifanya Pemba kufurika watu wakati wa msimu wa karafuu kwa ajili ya kuchuma zao hilo na wengine walikuwa wakitoka Unguja, kwa vile shughuli za kuvuna karafuu hufanywa kwa mikono.
Kazi ya kuchuma karafuu kwa kawaida hufanywa na watu wa rika zote wakiwemo wanawake na wanaume na wakati mwengine hata watoto wakati wanapokuwa hawendi kusoma.
Mara nyingi watu hutegemea sana kibarua cha kuchuma karafuu kupata mahitaji ya lazima, na hapo zamani vijana walikuwa wakiutumia msimu wa karafuu kupata mahari ya kuoa.
Wengine walitegemea uchumaji wa karafuu kwa kujenga nyumba, kusafiri, kusomesha watoto, kuondoa nadhiri, kununua mahitaji mbali mbali kama vile vyombo vya usafiri na kadhalika.
Kihistoria wakati wa msimu wa karafuu watu walikuwa wakijenga undugu wa kudumu baina ya watu wa Unguja na Pemba, kwa kuwa wengine walipata wake nyakati hizo za msimu wa kuchuma karafuu.
Misimu ya karafuu ilizidisha kukua kwa biashara za kuuza na kununua, kwani mbali ya ya waliokuwa wakija kwa maamuzi yao, lakini pia serikali ilikuwa ikishajiisha watu kwenda Pemba kuokoa zao hilo.
Marehemu Bambuti na ngoma yake ya Ndanda kule Donge Unguja, alikuwa akiimba nyimbo za kushajiisha watu kuokoa zao la karafuu kwa kusema “Twendeni Pemba ee! karafuu tukachume…….”
Kwa vile uokoaji wa zao la karafuu kushirikisha watu wote wanawake na wanaume, nilikuwa na shauku ya kutaka kujua namna watu walivyokuwa wanashindana katika uchumaji wa zao hilo na zaidi niliguswa na jinsi ya kike.
Nilipouliza baadhi ya watu maarufu katika kambi za karafuu, walinidokeza kuwa wapo wanawake maarufu katika uchumaji wa zao hilo na wakiwashinda wanaume.
Udadisi wangu ulizaa matunda na kuambiwa Wilaya ya Mkoani kuna mwanamke mmoja ana uwezo mkubwa wa kuchuma karafuu na kuwashinda hata wanaume.
Nilifunga safari hadi Manyaga, Wilaya ya Mkoani kuonana na mchumaji karafuu maarufu mwanamke ili kuzungumza nae juu ya ujasiri wake huo wa kuutataga mkarafuu na kupata mavuno mengi tafauti na baadhi ya wanaume.
Ni umbali wa kilomita kadhaa hadi kufika katika kijiji cha Manyaga, Shehia ya Mbuguani, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, lakini yote ni kufanikisha safari yangu ya kumuona mwanamke niliyesifiwa kuwa ni mwanamke wa shoka katika uchumaji wa karafuu.
Nilipofika kama kawaida nilimsabahi na kumuomba kuzungumza nae anipe mengi ya uchumaji wa karafuu katika enzi zake, kwani hivi sasa ni mtu mzima.
Nilianza kwa kumuuliza enzi zake ilikuwaje katika uchumaji wake wa karafuu na hata akawa maarufu na kuwashinda hata wanaume?
“Nikikumbuka enzi zangu na leo nilivyo kama kuna kuomba nirejeshewe umri fulani inakubaliwa basi mimi ningeliomba nirudi miaka 27 nyuma tokea kuzaliwa”, ni kauli ya mwanzo ya mama huyo, ambae kwa sasa ni mtu mzima mama.
Kauli hiyo imetoka kinywani mwa Bi. Heshima Khamis Ali, mwenye umri wa miaka 70 sasa , aliyezaliwa Mgagadu, Shehia ya Minazini, katika Wilaya ya Mkoani ,na kwa sasa ni mkaazi wa Manyaga, ambako ameolewa na mpaka leo hii licha ya kutengana na mume bado anakaa hapo hakuweza kuhama tena.
Bibi huyo kwa sasa ana watoto saba wakiwemo wanaume wawili na wanawake watano, ambao baadhi yao wameshakuwa wakubwa na wanachuma karafuu, ingawaje hakuna aliyemfikia katika kuchuma karafuu nyingi.
Bi. Heshima ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Mzee Khamis kati ya watoto watatu wawili ikiwa ni wa kike,ambapo wenzake walilelewa na bibi na babu kutokana na mapenzi ya wazazi kumsaidia mtoto wao ulezi.
Akielezea kwa upande wa wazazi wake hawakumbuki kuchuma karafuu bali wao walikuwa wanakaa nyumbani kwa ajili ya kushughulikia karafuu tu kwa kuanika, kufuata mahitaji ya vibarua na kuzishafisha karafuu na makonyo yanapokauka kwa sababu zilikuwa zinazaliwa kwa wingi na siku za mvua ushughulikiaji unakuwa mkubwa kuliko kuchuma.
“Wazazi wangu hawakuweza kuchuma wao ilibidi wabakie nyumbani mvua ikiwa kubwa inabidi kazi ya karafuu inakuwa kubwa na uwe mstahamilivu, na kama jua kali inabidi uwepo zinazopasi uondoe ili upate majamvi uanikie tena kwa sababu karafuu zinakuwa nyingi kama hukufanya hivyo zinaharibika zinakuwa mpeta (karafuu nyeupe) unakosa bei”, alisema.
ALIVYOANZA KUCHUMA KARAFUU

Akiielezea jinsi alivyoanza uchumaji wa karafuu alisema akiwa mdogo wa miaka minane wazee wake walikuwa wanamiliki mashamba ya mikarafuu, na hivyo alifundishwa na vibarua waliokuwa wanachuma katika mashamba yao namna ya kuchuma karafuu.
“ Kutokana na uzoefu huo niliendelea kuongeza kiwango changu cha uchumaji siku hadi siku kulingana na umri wangu ulivyoongezeka hadi kuwa na kasi zaidi ya uchumaji”, alifahamisha Bi Heshima.
Alisema ujasiri wake wa kuchuma haukuishia kwao alipokuwa mdogo, bali aliendelea nao mpaka pale alipoolewa ambapo alipofika kwa mumewe hali ilizidi kuendelea, kwani huko mikarafuu pia ilikuwepo na kulitokeza ushindani wa uchumaji wa zao hilo katika kijiji hicho.
“Huku nilikoolewa sasa naona ndiko nilipopata ari zaidi, kwani huku nilikutia wake wenza wawili nao pia walikuwa wachumaji kwa hiyo wayajua mambo ya ukewenza kwa hivyo tulikuwa twashindana haswa”, alisema Bi. Heshima kuonesha kuwa hakutaka kupitwa na wake wenza.
ANAVYOCHUMA KARAFUU
Alisema yeye kwanza alikuwa hachagui mkarafuu wa kupanda uwe mkubwa ama mdogo, lakini alikuwa anapendelea zaidi kuchuma mikarafuu mikubwa kwa sababu anapopanda juu ya mkarafuu alikuwa ndio amefika, huchukua zana zake zote ikiwemo maji ya kunywa na kipolo cha kumiminia.
Akizungumzia jinsi alivyoweza kuuchuma mkarafuu, alisema kwa upande wake yeye alikuwa anauanza kuuchuma chini ambako ndio kugumu mpaka akifikia kati kati.
“Nikifika hapo katikati inakuwa kwangu kama kuchukua chakula nakula wali na mboga kwenye mkeka wa Chole ama busati jipya kwa sasa”, alisema Bi. Heshima kunasibisha na tamathali hizo za semi.
“Siku ya mwanzo kuchuma kwenye mashindaoo ya ukewenza nilikwenda kutizama ustarabu (kusoma)wenzangu nguvu zao zikoje”, alisema.
Bi. Heshima (70) aliendelea kusema kwa vile kulikuwa na ushindani wa kuchuma, yeye ilikuwa anachuma mpaka anashindwa kuzichukua mwenyewe, kwa hiyo hupeleka ujumbe nyumbani na huletwa mtu na mumewe kuja kusaidiwa.
“Huletewa mtu hasa kutokana na mabonde na milima katika maeneo tuliokuwa tunachuma. Ama ataletwa punda au baiskeli kuchukua karafuu nilizozichuma kwa siku”, alisema.
Alifahamisha kuwa zinapofika nyumbani karafuu kwanza hawashughulikii kunyambua, bali huanza kupika, kufanya ibada sala ya alaasiri inawakutia njiani na baadae kula na wanapomaliza sala ya Isha ndio kazi ya kuchambua huanza kwa kusaidiwa na watoto wa mtaani.
Alibainisha kuwa uchambuzi wa karafuu kwa watoto waliupenda na ilikuwa zinamalizika haraka, kwani watoto hao walikuwa hawafuatii karafuu tu ilikuwa kunatolewa na Hadithi za Paukwa Pakawa na vitendawili.
“Wachumaji wa leo sijawasikia kutoa hadithi wala vitendawili na haya hivi sasa hayapo mabibi muda hatuna kwa watoto wetu na wajukuu waache watoto wamjue Zuchu na Daimondi watwambia wenda na wakati”, alisema Bibi huyo mwingi wa kusema.
Kwa upande wa malipo Bi. Heshima alisema kuwa kibarua pishi ilikua inachumwa shilingi ishirini (20. “Ilikuwa pesa ya noti rangi ya zambarau karafuu hazikuwa na pesa enzi hizo si kwa kibarua wala tajiri, lakini hicho kiliokuwa kinalipwa ilikuwa kinakidhi kutokana na mahitaji yaliokuepo, sambamba na mabadiliko ya awamu baada ya awamu mpaka kufikia leo hii ya pishi shilingi 2000”.
“Mimi muandishi ndio mwanzo nilipokuambia nirejeshwe miaka ya nyuma ningelikubali kwa sababu kwa wakati huu ingelikuwa nnaweza kuchuma kwa CARRY ningelinunua, lakini leo siwezi tena mwanangu, ”alisema.
Kwa upande wa watoto wake ambae amemrithi kwa kuchuma karafuu alisema ni mtoto wa tatu kuzaliwa anaeitwa Suleiman Mohamed Ali (33).” Ana uwezo wa kuchuma mpaka pishi 25 kwa sasa”, alisema.
KIPATO ALICHOKIPATA
Alielezea kuhusu kipato alichokipata kutokana na kazi yake hiyo, alisema ilitegemea na mzao unavyokuwa, ikiwa mzao mkubwa na mambo yanakuwa makubwa na ikiwa mdogo na inakua hivyo hivyo madogo,lakini kulingana na umahiri wa uchumaji wake hakuwa mkiani katika kipato.
“Bora mwanangu nisikutajie kima ninachokipata, lakini wa mwisho sitokei nikikwambia nitaambiwa najisifu nafikiri kushanielewa”,alisema.
Alisema alikuwa anachuma karafuu mpaka pishi 30 kwa siku, jambo ambalo halikuwa likimpa tabu kuchambua na kurejea tena kuchuma siku ya pili.
Bi. Heshima alisema kuwa katika uchumaji wake wa karafuu hakuishia huko tu alikoishi, bali pia aliwahi kuchuma katika sehemu nyengine ikiwemo Tironi, Shehia ya Mbuguani na Kichunjuu, shehia ya Mtambile zote katika wilaya ya Mkoani.
MAMBO ALIOYAPATA KUTOKANA NA UCHUMAJI WA KARAFUU
Kuhusu maendeleo yake aliyojifanyia kutoana na uchumaji wa karafuu , alisema amefanya mambo mengi ya kumasaidia.
“ Umaarufu wa kujuilikana na watu na nikiongozwa na aliyekuwa mume wangu aliniambia sote ni binaadamu tumeumbwa, kwa vile pesa ninayo baada ya kununua mahitaji yangu na kuwapelekea wazee chochote, nitafute kitu cha kuweka raslimali”, alisema.
“Kuanzia hapo nilianza kununua ng’ombe ambapo ninaendelea nao mpaka leo hii, nimejenga nyumba yangu, na ninamiliki shamba la mikarafuu ambalo ni la kwangu mwenyewe”, alifahamisha Bi. Heshima.
Alisema kwa vile alihamasika tokea mapema tokea kwa wazee wake walikuwa na mikarafuu, kwa hiyo nae alijenga ndoto hiyo na yeye amiliki shamba lake la mikarafuu na aliweza kuifikia alinunua ardhi ambayo ilikuwa haina mikarafuu na akaanza kuipanda sasa anafaidika nalo.
TAFAUTI YA UCHUMAJI WA ZAMANI NA SASA
Akitofautisha uchumaji wa karafuu wa zamani na hivi sasa, Afisa kutoka Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba, Maalim Khamis alisema uchumaji wa sasa na zamani unatafautiana, kwani zamani unaweza kulitembea shamba zima bila ya kukuta matawi yaliyokatwa ya mikarafuu.
Alisema hali hiyo ilionesha jinsi gani mti huu ulivyothaminiwa na waliomiliki na walijitahidi kuzungumza na wachumaji wao wasiivunje, kwani kufanya hivyo husababisha kila msimu unapowadia wa mwaka na Vuli uweze kuonekana na pande zote tatu ziweze kufaidika tajiri,mchumaji na kwa upande wa serikali ndio huduma za kijamii zinavyoimarika.
“Watu walikuwa wanatengeneza ngazi ndefu ambayo imegawika katika sehemu tatu chini, juu ya kati (matumboni ) na kileleni uchumaji huu unatumiwa na watu walioko nje ya mkarafuu bila kukerana na mwengine ambae yeye anakuwa ndani ya mkarafuu tofauti na sasa hivi kama unakwenda mabondeni unachanganyikiwa kwa mikarafuu inavyokatwa”, alisema.
WITO
Akitoa wito kwa jamii amesema katika miaka hii karafuu ilipopanda bei kumekuwa na tabia za ajabu tofauti na zamani, ambapo hivi sasa kunatokea mambo ya ajabu watu kuiba kwa kukata mikarafuu kwa mapanga, udhalilishaji mkubwa wa wanawake na watoto ikiwemo vitendo vya kikatili kudiriki hata watu kuchinjwa.
Aliiomba jamii kurejesha maadili yao ya zamani ya ukarimu kwa kuwakaribisha wageni, kwani ndio humo unamojengwa udugu na ndoa pia zilipatikana katika kipindi hicho.
“Sasa tuna mali kwa mali matajiri wameondoa imani kwa wachumaji wao, kwani kunatokea upoteaji mkubwa wa karafuu zao na baadhi mama wa kike wanadiriki kuzikanusha ndoa zao wanapokuwa mabondeni ili mradi warudi na karafuu”, alisema.
Alieleza “sijaonapo “Mpeta “ wa pishi tano tumezidi na watoto wakubwa (wari )wanakwenda mabondeni na simu wanaokota kwa mtandao maneno ya vijana”.
Aliiomba Serikali isaidie kuondosha wimbi la ukatwaji wa mikarafuu kwa mapanga, ununuaji wa karafuu mbichi mitaani, wizi unaozidi kuongezeka sambamba na utorokaji wa wanafunzi maskulini na katika vyuo vya Kur-ani.
“Katika maeneo ya ndani kumezidi hata usalama bararani haupo”, alifahamisha.
“Tunaokaa karibu na njia inapoingia asubuhi wanapotoka vibarua kuelekea mikarafuuni na jioni wanaporudi utaona kiwewe gari zinavyojaa na bodaboda moja inachukua watu mpaka watano huwezi kuangalia,”alisema.
Bi. Heshima ni mama amechuma Karafuu katika maeneo mbali mbali katika Mkoa wa Kusini Pemba ikiwemo Tironi Shehia ya Mbuguani na Kichunjuu Shehia ya Mtambile Wilaya ya Mkoani Pemba.