WASHINGTON, MAREKANI

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewaambia wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa tishio kwa amani na usalama.

Blinken alirejelea athari zinazofurika za mabadiliko ya tabia nchi kwa karibu kila nyanja ya maisha kuanzia kilimo, miundombinu, afya ya umma hadi usalama wa chakula.

Blinken alisema wanachama wanapaswa kuacha kujadiliana ikiwa janga la tabia nchi ni la Baraza la Usalama.

Aliongeza kuwa wanatakiwa kuuliza ni kwa namna gani baraza hilo linaweza kutumia nguvu zake za kipekee kukabiliana na athari hasi za tabia nchi kwa amani na usalama.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Raychelle Omamo alisema mabadiliko ya tabia nchi yanasababisha hali kuwa mbaya zaidi katika maeneo yenye migogoro barani Afrika na kuongeza kuwa, Operesheni ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika maeneo hayo pia inapaswa kushughulikia athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye umoja huo Zhang Jun alisema, wanapaswa kusema kuwa si nchi zote kwenye ajenda ya baraza hili zilikumbwa na machafuko kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi.