NA LAYLAT KHALFAN
KIKOSI cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU), kimesema kutolewa kwa elimu ya kujikinga na majanga mbalimbali ya moto itawezesha jamii kuchukua kinga za tahadhari pindi inapotekea majanga hayo.
Ofisa Mkaguzi wa Kikosi hicho, Haji Khatib Hassan, aliyasema hayo wakati akiwapatia mafunzo ya kujikinga na majanga ya moto na utumiaji wa vifaa vya kuzimia moto kwa wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi.
Alisema ili jamii iweze kujikinga na majanga hayo kikosi hicho kinachukua jitihada za makusudi kupita kila taasisi kwa ajili kutoa elimu sahihi ya kujiepusha na majanga kama hayo.
Alisema mafunzo hayo ni moja kati ya majukumu makubwa ya kikosi hicho na nimwendelezo wa kutoa elimu kwa taasisi za serikali, binafsi na wananchi kwa ujumla.
“Ndani ya jamii zetu mara nyingi kunatokea majanga ya moto na kuathiri mali na watu hivyo tukitoa elimu hii mara kwa mara katika maeneo tofauti itasaidia kupunguza athari kubwa zinazotokezea”, alisema.