NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu Tanzania imesema kuwa ukuaji wa uchumi wa dunia unaimarika kwa kasi ndogo kutokana na uwepo wa janga la ugonjwa wa corona na kwamba kwa siku za usoni uchumi huo utaimarika zaidi.

Gavana wa benki hiyo, Prof. Florens Luoga alieleza hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, ambapo alisema kutokana na kikao cha 216 cha kamati kilichokutana kimetathmini utekelezaji wa sera ya fedha na kupitia mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia.

Alisema mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania bara na Zanzibar kwa robo ya kwanza ya mwaka 2021, ulikuwa wa kuridhisha, ambapo kwa Tanzania bara, ulikuwa kwa asilimia 4.9, ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2020 na Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 2.2 ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.5 katika robo ya kwanza mwaka jana.

Alisema ukuaji wa uchumi huo kwa Tanzania bara umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, uchukuzi, kilimo, uzalishaji viwandani na uchimbaji wa madini.

Alieleza ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuendelea kuimarika kwa Tanzania bara na Zanzibar, kutokana na uwekezaji unaoendelea katika miradi mbali mbali ya serikali na kuimarika kwa uchumi wa dunia, ambapo hali hiyo itachochea uwekezaji katika sekta binafsi na biashara.

Hata hivyo alisema kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha mwezi Julai na Agosti mwaka huu, ambao uliwezesha uwepo wa ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki, hali iliyojidhihirisha katika viwango vya riba katika masoko ya fedha ambavyo vimeendelea kubaki kati ya asilimia 3.5.

Aidha alifahamisha kuwa, mikopo kwa sekta binafsi ilikuwa kwa asilimia 4.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu, kutoka asilimia 3.6 kwa mwezi uliotangulia.

Aliongeza kusema kwamba, sekta ya nje imeendelea kukabiliwa na changamoto zitokanazo na UVIKO-19, hususani katika sekta ya utalii.

Kwa upande wa mauzo ya dhahabu yameongezeka na kufikia dola bilioni 3, kwa mwezi ulioishia Julai 2021, ambapo akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha na kufikia dola bilioni 5.5, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 6.