TUNIS,TUNISIA

SPIKA wa Bunge ambaye pia ni mkuu wa chama cha An Nahdhah cha Tunisia amesema anatarajia kuwa mazungumzo ya kitaifa yataanza chini ya usimamizi wa Rais Kais Saeid wa nchi hiyo.

Akizungumzia matukio ya karibuni nchini Tunisia Rached Ghannouchi alisema,anatarajia kuwa pande kuu za kisiasa nchini humo zitakutana ili kuanza mazungumzo ya kitaifa chini ya usimamizi wa Rais Kais Saeid ili kutatua mgogoro unaoikabili nchi hiyo.

Ghannouchi alisisitiza kuwa, mazungumzo yasiyo na vizuizi ni jukwaa zuri kwa ajili ya kutafuta suluhisho la matatizo ya sasa.

Kuhusu mafaili ya ufisadi nchini Tunisia, mkuu huyo wa chama cha An Nahdhah alitaka yawasilishwe katika vyombo vya mahakama bila ya kuhusishwa na mchezo wowote wa kisiasa.

Januari 25 mwaka huu Rais wa Tunisia alimfuta kazi Waziri Mkuu,Hicham Mechichi na kusitisha shughuli za bunge sambamba na kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria baada ya kupamba moto mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Akizungumza na waandishi habari, Rais Saied aliahidi kuunda serikali mpya haraka iwezekanavyo itakayokuwa na viongozi wenye uwezo wa kiutendaji na si kwa kujuana au kwa utashi wa kisiasa.Pamoja na hayo alikataa kutangaza tarehe hasa ya kuunda serikali hiyo.