Yasema wanasimamia vyema dhamana zao

NA ASIA MWALIM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema kimeridhishwa na utendaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Peter Nao, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari, katika ofisi kuu ya CCM, Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Alisema hatua hiyo inatokana na tathmini iliyofanywa na kamati maalum ya halmashauri kuu ya taifa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Dk. Ali Mohamed Shein, iliyojadili utendaji kazi wa viongozi hao.

Aidha alisema kutokana na juhudi zinazochukuliwa na viongozi hao jinsi wanavyoshughulikia masuala ya kujenga nchi kwa dhamana zao walizopewa.

Alisema viongozi hao wanaendelea kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo kwa kuamua kwenda mbele zaidi na kutangaza Utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi ili watu wafahamu rasilimali zilizokuwemo ndani ya nchi hii.

“Kwa mara ya kwanza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ameshughulika kutangaza visiwa vya Zanzibar kupitia rasilimali zake, amezindua maeneo ya Kizimkazi pia ataendelea katika maeneo mbali mbali ya Tanzania ili kuimarisha utamaduni wa nchi,” alieleza Catherine.

Alisema CCM imeona utendaji wa mama Samia kusikia kilio cha wananchi kuhusiana na suala la tozo na kushughulika nalo jambo ambalo limetoa faraja kuona Tanzania inakwenda na wananchi wakishughulikiwa matatizo yao.

Catherine alisema kuwa imeshuhudiwa kwa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshuhudiwa Rais wa nchi hizo kukaa kuzungumzia masuala ya muungano na kubainika hoja 11 ambazo zinatakiwa kushughulikiwa.

Kwa upande wa Rais wa Zanzibar, Catherine alisema kamati maalum imeridhishwa na namna anavyosimamia vyema suala la fedha za umma kwa kudhibiti matumizi yasiyo sahihi sambamba na kuzuia fedha hizo kuchezewa.

Aidha aliongeza kuwa CCM imeridhishwa na jinsi anavyoshughulikia nidhamu ya wafanyakazi na kuhimiza uwajibikaji hali iliyoongeza ufanisi na watendaji kuacha kufanya kazi kimazoea.

“Kamati hiyo imeona utekelezaji wa Dk. Mwinyi, jinsi anavyoshughulikia suala la dawa za kulevya ikiwemo kuanzisha mahakama maalumu ya watu wanaohusika na kadhia hiyo ili kupunguza na hatimae kuondoa kabisa suala hilo kwa upande wa Zanzibar kunusuru vijana wetu,” alieleza Katibu huyo.

Kuhusiana na suala la udhalilishaji Catherine alisema, kamati imeridhishwa na jinsi linavyoshughulikiwa hata hivyo aliwataka viongozi wa dini kuangalia kwa makini viongozi wanaowapa dhamana ili kuunga mkono juhudi za Dk. Mwinyi katika kuondoa suala la udhalilishaji Zanzibar.

Alisema kamati imeridhika na viongozi hao kukagua miradi mbalimbali iliyoanzishwa ili kujiridhisha na ikibainika ina tija inaweza kukubaliwa, pia kuibua na kuiendeleza miradi mipya.

Hata hivyo alisema Chama cha Mapinduzi kupitia kamati maalumu imeridhishwa na suala la uwajibikaji wa viongozi hao wakuu, kubaini kuwa wanafaa kuendelea kubaki madarakani kulingana na ufanyaji kazi wao wa dhati ili kushuhudia mambo mengine yanayoendelea.

Katika hatua nyengine Katibu huyo alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mchakato wa kuona wanampata mgombea wa Jimbo la Konde ili kufanya uchaguzi wa kistaarabu.