NA KIJA ELIAS, MWANGA
SERIKALI imewataka Wataalamu wa mazingira kufika katika ziwa Jipe lililopo wilaya ya Mwanga, kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini sababu za kuwepo kwa magugu maji yanayosababisha maji kupungua pamoja na viumbe hai kuhama katika ziwa hilo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Chande, alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake alipotembelea ziwa hilo kwa lengo la kukagua uharibifu huo.
Akiwa katika ziara hiyo ambayo aliambatana na viongozi wa NEMC, Chande aliwaagiza wataalamu wa mazingira kufika haraka katika ziwa hilo na kujiridhisha namna ya hali ya ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu ili kuweza kuandika maandiko mbalimbali ya miradi ili kupata fedha kutoka kwa wafadhili na washirika wa maendeleo.
“Serikali haina budi kuleta wataalam katika ziwa hili ili waweze kuja na kufanya tathimini za kina juu ya athari za uwepo wa haya magugu maji katika ziwa hili,”alisema Chande.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Tadayo, ameiomba serikali kupeleka wataalamu kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina ili kuja na majibu ambayo yatasaidia kubaini chanzo cha magugu maji hayo.
Tadayo alisema ziwa Jipe ndiyo chanzo kikubwa cha maji yanayotegemewa katika mradi mkubwa wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe unayotekelezwa na serikali.
“Ziwa Jipe lina umuhimu mkubwa sana kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe, maji hayo yanakwenda katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambako pia umeme unazalishwa huko, hivyo kama serikali haitavilinda vyanzo hivi miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha nyingi baada ya muda haitakuwa na tija,” alisisitiza Tadayo.