NA HAFSA GOLO
WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imepokea vifaa vya upasuaji wa maradhi ya ngiri kutoka serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China, ambavyo vimegharimu zaidi ya shilingi milioni 32.
Akikabidhiwa vifaa hivyo, mkurugenzi mkuu wa wizara ya Afya, Dk. Abdulla Suleiman Ali alisema vifaa hivyo vitatumika katika hospitali ya Chakechake kisiwani Pemba na hospitali ya Kivunge iliyopo wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Alisema vifaa hivyo vilivyotolewa msaada vitatumika kwa wagonjwa 400 wanaosumbuliwa na maradhi ya ngiri, ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.
Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya China imekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia sekta ya afya nchini ambao mbali ya vifaa tiba, pia imekuwa ikisaidia dawa za kutibia maradhi mbalimbali.
“Msaada huo tuliopokea ni endelevu kwa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Wizara tunatambua juhudi zao katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi”, alisema.
Naye Daktari Dhamana wa hospitali ya Kivunge, Tamim Hamad Said alisema kwa upande wa Kaskazini Unguja tatizo la maradhi ya ngiri ni kubwa na wapo baadhi ya wagonjwa wenye kuhitaji kufanyiwa upasuaji.
Alifahamisha kwamba kuregea masuli za tumbo pamoja na kubeba mizigo mizito kunasababishwa mwanamme kupata maradhi ya ngiri.
Kwa upande wake Balozi Mdogo wa Serikali ya China Zhang Zhisheng alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa katika huduma za afya ili kuona hali za wananchi zinaimarika.
Alisema serikali ya China itaendelea kudumisha uhusiano wa kidugu baina ya serikali mbili hizo kwa kuondosha changamoto mbali mbali.