NA MWANDISHI WETU, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema maeneo kadhaa ya visiwa vya Zanzibar yanakabiliwa na changamoto ya kimazingira kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Makamu alieleza hayo jana huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa shirika la Afrika Kusini la CITY CON Africa, linaloshughulikia mipango miji na utunzaji mazingira.

Ujumbe huo ulikutana na Makamu wa rais wa Zanzibar kubadilishana mawazo na kuwasilisha wazo la kuanzisha mradi wa ufukiaji ardhi katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar ili yaweze kutumika kwa shughuli za uwekezaji miradi ya kiuchumi, uhifadhi wa mazingira na kusaidia kuongeza mapato na kukuza maendeleo ya nchi.

Othman alifahamisha kwamba, kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, Zanzibar imetayarisha mpango mkuu na sera ya kulinda mazingira ili kunusuru janga linaloendelea la mabadiliko ya tabianchi.

Makamu alikaribisha wazo la shirika hilo la kuanzisha mradi wa ufukiaji ardhi utakaozingatia kuepuka changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na pia kasi kubwa ya ongezeko la idadi watu na uharibifu wa mazingira linalochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja Juma, alisema kwamba tafiti zilizofanywa zimebaini Zanzibar kuwepo maeneo mbali mbali yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kwamba athari hizo zipo katika sekta mbali mbali zikiwemo kilimo, uvuvi na pia kuharibika mfumo na mtiriritiko wa miongo na upatikanaji wa mvua, kina cha bahari kuongezeka na hivyo kuchangia kupunguza kasi na juhudi za kiuchumi nchini.

Awali mwakilishi wa kampuni hiyo Simbarashe Manwere, alimueleza, Makamu kwamba Shirika la City Con Afrika lipo tayari kushirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau wengine kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema shirika hilo lipo tayari kuanzisha mradi mkubwa wa ufukiaji ardhi Zanzibar ili itumike katika shughuli za uwekezaji na kuongeza mapato na kuchangia kukuza uchumi wa Zanzibar.