Wageni wanaotembelea makumbusho wapungua

 Idara yataka mkazo uwekwe kuhamasisha utalii wa ndani

NA ASYA HASSAN

TANGU mwenzi Disemba mwaka 2019 kwa mara ya kwanza ulipobainika ugonjwa wa corona katika mji wa Wuhan nchini China na kusambaa karibu sehemu zote za dunia, hadi sasa ulimwengu unaendelea kuuguza ugonjwa huo.

Mataifa yamechukua juhudi mbalimbali katika kudhibiti ugonjwa huo, ikiwemo karantini ya raia wao kutoka nchi moja kwenda nchi nyengine, ambapo karantini hiyo ilihusu watu kutoka mji mmoja kwenda mji mwengine ndani ya nchi moja.

Katika baadhi ya nchi karantini ilikuwa kali zaidi kwani ilikuwa marufuku watu kutoka majumbani mwao hasa nyakati za usiku na hata wale wanaopenda starehe za usiku, vilabu vilifungwa kukwepa maambukizi.

Takwimu za hivi karibuni kabisa zinaonesha kuwa ugonjwa huo umeambukiza zaidi ya watu 230, 326, 827, kati ya hao walioambukizwa watu 207,033,588 wameripotiwa kupona, ambapo taarifa zinabainisha kuwa watu wapatao 4,722,911 duniani kote wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Kwa hakika ugonjwa wa corona umesababisha taharuki kubwa kijamii na zaidi kiuchumi kwa nchi mbalimbali hasa kwenye sekta ya utalii ambayo ni miongoni mwa biashara yenye kuingiza fedha nyingi duniani.

Zanzibar ikiwa sehemu ya ulimwengu nayo imeathiriwa kwa kiasi kukibwa kutokana na ugonjwa wa covid 19, kwani baadhi ya famialia zimewapoteza ndugu, jamaa, marafiki na wapendwa wao kutokana na janga la maradhi hayo.

Hapana shaka yoyote ugonjwa wa corona pia umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii, ambayo ni miongoni sekta kiongozi kwa uchumi wa visiwa hivi hasa kutokana na karantini zilizowekwa katika nchi za nje za kuzuia watu kusafiri.

Utalii wa Zanzibar unajumuisha kuweko kwa fukwe nzuri na zenye kuvutia, mapango na majengo ya asili pamoja na vitu adimu ambavyo haviwezi kupatikana nchi yoyote ile duniani.

Sambamba na hilo, lakini msitu wa hifadhi ya Taifa wa Jozani kwa Unguja na msitu wa hifadhi wa Ngezi uliopo kisiwani Pemba ni miongoni mwa vivutio vya kitalii hapa Zanzibar.

Aidha makumbusho yenye vitu vya kale kama jumba la wananchi, makumbusho ya Mnazimmoja, Unguja Ukuu nakadhalika ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na watalii.

Katika makala haya tutazungumzia namna ya makumbusho yalivyopungukiwa na idadi ya matembezi ya watalii hasa kipindi cha wimbi la kwanza la ugonjwa wa corona, ambapo hadi sasa hali ni ya kusuasua kuingia kwa watalii.

Wakizungumza na makala haya baadhi ya maofisa kutoka kitengo cha hesabu cha Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar, ambao hawakutaka majina yao yatajwe wanasema ugonjwa wa corona umesababisha kushuka kwa makusanyo ya fedha zinazotokana na wageni wanaoingia nchini kutembelea maeneo ya kihistoria zikiwemo makumbusho.

Maofisa hao wanasema kutokana na hali hiyo Idara hiyo katika kipindi cha covid 19 awamu ya mwanzo ilifanikiwa kukusanya wastani wa shilingi 43,859,144 kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka 2020.

“Fedha hizo ni kutokana na tozo za wageni na wenyeji mbalimbali waliyoingia ndani ya maeneo hayo kwa kipindi hicho,” wanasema.

Kitengo hicho kinasema makusanyo hayo ni madogo ukilinganisha na miaka ya nyuma kwasababu kipindi cha maradhi hayo hakukuwa na wageni waliyoingia hapa nchini.

“Kipindi kile kulikuwa hakuna wageni waliyoingia haliambayo ilisababisha serikali kukosa mapato mengi yanayotokana na sekta hiyo,” wanasema.

Wakizungumzia takwimu za wageni waliyoingia ndani ya kipindi hicho maofisa hao wanasema wageni na wenyeji 11,401 walitembelea katika maeneo hayo.

Wanafahamisha kwamba idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo hakukuwa na tatizo lolote katika nchi au dunia kwa ujumla.

Kwa upande wa Msaidizi Kitengo cha Uwenezi na masoko kutoka Idara hiyo Zuhura Ally Juma, anasema maradhi ya corona yamechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa makusanyo ndani ya Idara hiyo kutokana na kipindi chote cha maradhi hayo hakukuwa na wageni waliyoingia hapa nchni.

Anasema kutokana na hali hiyo ipo haja kwa serikali kuzidi kuutangaza utalii wa ndani kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato pale kunapotokea tatizo kama hilo.

“Uingiaji mkubwa wa wageni ndio unaosaidia kuinua mapato hapa nchini kutokana na wenyeji hawana mwamko wa kutembelea maeneo hayo na pia hawana kiingilio katika eneo hilo na badala yake wanachangia kwa asilimia ndogo sana,” anasema.

Sambamba na hayo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuyaimarisha na kuyatangaza maeneo hayo pamoja na kuutangaza utalii wa ndani, ili wananchi waweze kuvutika na kuyatembelea.

Anasema endapo kupatikana kwa fedha za kutosha zitasaidia kuyabadilisha maeneo hayo kwa kuweka vitu vingine ili yazidi kuvutia.

Anafahamisha kuwa maeneo ya historia na nyumba za makumbusho hazina mabadiliko kutokana na kukosekana fedha za kuyabadilisha licha ya kuwepo wabunifu na wataalamu wa kufanya hivyo.

Zuhura anafahamisha kwamba hali hiyo imesababisha maeneo hayo kukosa mvuto wa kutembelewa na wananchi wa ndani.

Aliishauri serikali kuweka fedha ili ziweze kutumika katika kuyabadilisha maeneo hayo pamoja na kubuni maonesho ya muda mfupi ili watalii wanapoingia waweze kuvutika pamoja na kuwavutia wazawa.

Alisema licha ya makumbusho hizo kuwa na vitu tofauti vya kuvutia lakini zinahitaji kuimarishwa na kuwekewa miundo mbinu imara na kuongezewa ubunifu mpya ili zizidi kuvutia, hivyo ni vyema serikali kuongeza bajeti ili kupatikane fedha za kutosha ili kufanikisha ubunifu huo.

Akizungumzia suala la utalii wa ndani Zuhura alisema eneo hilo halijatangazwa ipasavyo kutokana na idara haina rasilimali fedha kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo.

Sambamba na hayo alisema maeneo hayo yanauwezo mkubwa wa kuingia fedha nyingi serikali zitakazosaidia kuinua uchumi wa nchi hivyo ni vyema kushulikiwa ipasavyo pamoja na kuwekewa mikakati imara ili kuleta tija hapa nchini.

Hata hivyo Zuhura alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kuwa na utamaduni wa kwenda kutembelea maeneo hayo ili waweze kujua historia mbalimbali ziliyopo nchini kwao.

Kwa upande wa Mkuu wa kitengo cha Mambo ya Kale, Abdalla Khamis Ali, anasema ipo haja kwa serikali kuangalia upya bei za kuingilia katika maeneo ya kihisoria kwa wazawa ili kusaidia kuongeza mapato ya serikali.

Anasema ni vyema serikali ikaangalia uwezekano wa kubadilisha bei za kiingilio katika maeneo hayo ili kusaidia kuongeza mapato serikalini.

Mkuu huyo anafahamisha kwamba kiwango cha kiingilio kwa sasa ni kidogo ukilinganisha na thamani inayopatikana kupitia maeneo hayo, hivyo ni vyema kuangaliwa upya ili kiweze kukidhi mahitaji, hususani katika kipindi kama hicho kunapotokezea matatizo kama hayo.

“Kwenye maeneo hayo kunapatikana vitu mbalimbali ikiwemo elimu, mapumziko, historia ni maeneo ambayo yanahitaji kuangaliwa na serikali ili kuona yanaingiza mapato ya serikali”, alisema.

Aidha anafahamisha kwamba wazazi na walezi wanatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwalipia watoto wao kwa ajili ya kwenda safari hizo lakini fedha zinazolipwa katika maeneo hayo ni kidogo.

“Iwapo utalii wa ndani utatiliwa mkazo ni wazi kuwa itaacha hata kutgmea wageni kutoka nje, lakini kwa sasa nguvu nyingi zimeelekezwa kwa wageni kukitokea jambo la kuwafanya wageni wasije nchi inaathirika kama hivi sasa corona”, alisema.

Anasema utaratibu wa serikali kwa wazawa ni kulipa kiasi kidogo cha fedha huku akitilia mfano wa wanafunzi wanapotembelea kwa wingi hulipa kima cha shilingi 3000 tu kwa wote huku mtu mzima wa kawaida akilipa shilingi 1,000, kiwango ambacho hakina maslahi na hakileti tija.

Alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuangalia suala hilo kwa upana na umuhimu wake ili kusaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ndani hususani pale kunapotokezea matatizo kama hayo.

Mbali ya hayo lakini pia serikali imeshaanza kutoa chanjo kwa baadhi ya watoa huduma katika maeneo mbalimbali hatarishi ikiwemo watoa huduma wa afya, wafanyakazi wa bandari, uwanja wa ndege na maeneo mengine.

Kwa kuwa ugonjwa wa corona ni janga la dunia na Zanzibar kama sehemu ya dunia inabidi kufuata utaratibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) ili kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kuchanja chanjo ya corona.