BARCELONA, Hispania
KIUNGO mshambuliaji raia wa Brazil, Philipe Coutinho, anatazamwa kama mchezaji wa kipekee ambaye atakuwa na nafasi kubwa ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona na kurejesha umuhimu wake msimu huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Marca la Hispania, Coutinho sasa anatarajiwa kucheza mechi nyingi zaidi chini ya kocha, Ronald Koeman, kikosi ambacho kwa siku za hivi karibuni kimeonekana kupungua ubora.
Coutinho amerejea akiwa fiti na tayari ameshaanza kucheza mechi na kikosi chake cha Barcelona akitokea benchi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo walipoteza, dhidi ya Bayern kwa mabao 3-0.
Mshambuliaji huyo anamaliza mkataba wake wa sasa na Barcelona mwaka 2023, na msimu ujao utakuwa muhimu zaidi katika maisha yake ya soka ili kujua hatma yake.
Barcelona wanaweza kufanya uamuzi msimu ujao wa majira ya joto, ikiwa wasalie na nyota huyo au wamuweke sokoni.
Nyota huyo alitumia mwaka mmoja kwa mkopo akiwa na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich, akifanikiwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kujikuta kwenye mkwamo kutokana na majeraha na hakuwa kwenye kiwango kizuri.
Wakati huo huo, Barcelona ilikataa ofa ya pauni milioni 85 kutoka Manchester United kwa ajili ya uhamisho wa mshambuliaji yoso, Ansu Fati, katika dirisha la uhamisho la msimu wa majira ya joto wa 2020.Yoso huyo alifunga magoli matano na kutoa usaidizi mar nne kwenye mechi 10 katika michuano yote mwaka jana kabla ya kupata maumivu makubwa la goti ambayo yalimuweka nje ya uwanja kwa miezi 10.
Kiwango cha nyota huyo katika msimu wa 2019-20, kiliwavutia United na kuamua kutuma ofa Camp Nou.Kwa mujibu wa AS, ‘mashetani wekundu’ hao waliwasilisha ofa ya pauni milioni 85 kwa ajili ya huduma ya nyota huyo, wakati huo walikuwa wakijaribu kumsajili, Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.
Barcelona inasemekana ilikataa moja kwa moja ofa hiyo, na kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer badala yake kikawekeza dau la pauni milioni 73 kwa Sancho katika msimu wa majira ya joto wa 2021.Mkataba wa Fati uliopo Barcelona unafika mwisho msimu ujao wa majira ya joto, lakini, miamba hiyo inaripotiwa kuwa na imani ya kumshawishi nyota huyo wa kimataifa wa Hispania kukubali mkataba mpya.(Marca).