NA HAFSA GOLO

BARAZA la Kuwawakilisha watumiaji wa huduma za Maji na Nishati (CRC), limeviomba vyombo vya habari kushirikiana kufichua changamoto zinazowagusa watumiaji na kufikia azma ya kuanzishwa kwa chombo hicho.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Hadiya Abdurahman Othman, alieleza hayo hivi karibuni alipokua akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati, Zanzibar   (ZURA), Maisara Unguja.

Alisema iwapo wanahabari watashirikiana kwa pamoja  katika kuibua changamotozo zinazowakabili wananchi wanaotumia huduma ya maji na nishati   upo uwezekano mkubwa ya kufikia malengo ya serikali kwa muda muwafaka  ya kuundwa kwa chombo hicho chenye dhamira ya kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za maji na nishati Zanzibar.

Aidha alisema ili chombo hicho kiweze kuleta mabadiliko katika usimamizi wa maslahi ya watumiaji kunahitajika nguvu za mashirikiano baina ya watendaji na wananchi wote hasa ikizingatiwa eneo hilo linagusa watu wote.

Alibainisha miongoni mwa misingi ya utendaji kazi ya chombo hicho alisema  ni kuhakikisha kunakuwa na nidhamu,uwazi na uwajibikaji,ubunifu,kujitolea ,ujumuishaji na ufahamu wa mabadiliko ya hali ya nchi.

Sambamba na hilo alisema miongoni mwa haki na wajibu wamtumiaji wa huduma hizo ni pamoja na kulindwa  kutokana na bidhaa au huduma ambazo ni hatarishi kwa afya ya mtumiaji.

Nao baadhi ya wanahabari walioshiriki  mkutano huo walilihakikisha kufanya kazi kwa pamoja ili kuona kunakuwa na mabadiliko yaliokusudiwa na serikali ikiwa ni pamoja na watumiaji wanaweza kutumia chombo hicho ili waweze kupaza sauti zao.