NA AMINA AHMED, PEMBA

ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha CUF aliyeondolewa madarakani na baadae kutangaza kurudi kuchukua nafasi yake, Abass Juma Muhunzi amemtaka mwenyekiti wa chama hicho Prof.  Ibrahim Haruna Lipumba kujiuzulu.

Akizungumza na waandishi wa habari kisiwani Pemba, Muhunzi alisema Prof. Lipumba anapaswa kujiuzulu kwenye nafasi yake ya uenyekiti wa CUF kwa kile alichodai kuwa amevunja katiba ya chama.

Makamu huyo alisema Prof. Lipumba anatumia vibaya madaraka kwa kujichukulia maamuzi yenye maslahi binafsi pasi na kuangalia maslahi ya chama jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya chama hicho.

Muhunzi alisema mwenyekiti huyo ameshindwa kutekeleza vyema majukumu yake kwa kutoitendea haki nafasi kubwa ya uongozi aliyonayo katika chama na hivyo kukiyumbisha chama upande wa Zanzibar.

“Wananchi wanakumbuka baada ya migogoro na chama kugawanyika wengine wakaenda ACT na sisi wengine tuliamua kubaki katika chama hichi, tulidhani tuko njia moja, lakini kumbe Lipumba ana figisufigisu tulivyomfikiria sivyo alivyo”, alisema.

Aliendelea kusema kuwa Prof. Lipumba yupo kwenye chama hicho kwa ajili ya kujipatia fedha tu kuendeshea miradi yake, ambapo hali hiyo imedhihiri kwa kiasi kikubwa kwa chama hasa upande wa Zanzibar kwa kutopata mgao wa fedha za uendeshaji.

Aidha alieleza kuwa mwenyekiti huyo amekuwa akizipuuza hoja zinazotolewa katika vikao vinavyojadili changamoto za uendeshaji wa chama hususani upande wa Zanzibar   na kupelekea kukishusha hadhi chama hicho kwa wananchi.

Kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa chama hicho Mussa Haji Kombo alisema endapo mwenyekiti huyo ataendelea kubaki katika chama kitazidi kupoteza hadhi kwa wananchi kwa vile kiongozi huyo anasababisha migogoro.

Naye Ali Makame Issa ambae alikuwa naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, alisema mwenyekiti huyo amekuwa akirudisha nyuma harakati za wanachama kutokana na kutofuata katiba sambamba na kuchukua maamuzi ya peke yake.