NA VICTORIA GODFREY

WANACHAMA wa klabu ya Simba  wa Tanzania Bara ,Zanzibar na nje ya Tanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono Tamasha la  Simba day, ambalo limepangwa kufanyika Septemba 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.

Rai hiyo imetolewa na aliyekuwa mwenyekiti wa Simba na muasisi wa tamasha hilo Hassan Dalali  wakati akizungumza na gazeti hili.

Alisema siku hiyo itatumika kumuenzi aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo Hans Popo,kufanya utambulisho wa wachezaji waliosajiliwa msimu mpya .

Alisema ushiriki mkubwa wa wanachama na mashabiki utasaidia kuwapa ari  wachezaji kujipanga kuelekea msimu mpya  wa ligi kuu Tanzania Bara inayotarajia kuanza kutimua vumbi mwezi huu.

“Tunaomba wanachama wa ndani na nje ya nchi wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia, kwani siku hiyo  itakuwa ya kukatana shoka na tofauti na matamasha yaliyopita kama hilo,” alisema Dalali

Aidha aliipongeza kamati ya usajili na wanaimani kikosi hicho kitafanya vyema msimu ujao wa ligi.

” Kamati ya usajili tunaamini na tutakuwa na kikosi bora cha ushindani msimu huu, ambacho kitaleta matokeo mazuri msimu ujao,” aliongeza Dalali.