NA JUMBE ISMAILLY, IGUNGA    

ZAIDI ya watu 70,000 wanaoishi katika Kata tano zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora,  wamekuwa wakiathirika kiafya, kielimu pamoja na kiuchumi kutokana na kukatika kwa daraja la Mto Mwamashiga katika kipindi mvua zinapoanza kunyesha.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Igunga, Mhandisi Sadick Karume, alisema kutokana na kukatika kwa daraja hilo kwa kipindi cha miaka miwili sasa, hivyo serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo unaotarajia kuanza mwezi Novemba mwaka huu.

Mhandisi huyo alikuwa akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo kwa Mbunge wa jimbo la Igunga, Nicholaus Ngasa, aliyekuwa katika ziara ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Karume ujenzi wa daraja hilo lililobomoka kwa zaidi ya miaka miwili sasa, unatarajia kukamilika kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 350.

“Kiasi hicho cha fedha ni kati ya shilingi bilioni moja na nusu kilichotengwa kwa ajili ya kutengeneza daraja hilo na mengine mawili pamoja na barabara zinazounganisha Kata” alisisitiza Mbunge Ngassa.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo,Mbunge wa jimbo la Igunga, Nicholaus Ngassa, alibainisha kwamba daraja hilo limekuwa likikata mawasiliano ya kata Tano, wakati wa masika na kuzitaja kata hizo kuwa ni pamoja na Itunduru, Igurubi, Ntobo, Kinungu na Mwamashiga na hivyo kuwaathiri wananchi kiuchumi, kiafya na kijamii.

Aidha, Mbunge Ngassa, alitumia fursa ya zira hiyo kuishukuru serikali kwa utaratibu wa wabunge kuchagua barabara na madaraja ya kutengenezwa, na kwamba wamelipa kipaumbele daraja hilo pamoja na barabara zinazounganisha kata hizo.

“Tunataka wananchi wanaoathirika na kukatika kwa daraja hilo hususani kipindi cha masika, kipindi ambacho hivi sasa ndiyo kinakaribia, waondokane na adha hiyo”alifafanua Ngassa.