WASHINGTON, MAREKANI

KAMPUNI kubwa ya kutengeneza dawa ya Marekani ya Pfizer imesema kwamba imeanza majaribio ya dawa inayolenga kulinda watu wanaoishi na mtu aliyeambukizwa corona.

Dawa hiyo inalenga kuwazuia wasiokuwa na dalili zozote za maambukizi dhidi ya kupata virusi hivyo.

Dawa hiyo ambayo ni ya kumezwa itafanywa majaribio kwa watu 2,660 wenye afya nzuri na ambao wameishi katika nyumba moja na mtu aliyewahi kupata corona.

Pfizer pia inafanya majaribio ya dawa hiyo kwa watu ambao tayari walipata corona ingawa hawajaonesha dalili zozote za maambukizi.

Mkuu wa utafiti wa kisayansi kwenye kampuni hiyo Dkt Mikael Dolsten alisema kwamba iwapo dawa hiyo itafaulu, basi huenda ikadhibiti virusi vya Covid-19 kabla havijaenea zaidi.

Wakati huo huo, rais wa Marekani Joe Biden amepokea chanjo yake ya tatu maarufu kama booster muda mfupi baada ya utawala wake kuidhinisha hatua hiyo kwa makundi maalum ya watu.

Muda mfupi kabla ya kupokea chanjo hiyo, Biden alisema ni muhimu kupata chanjo hiyo ya tatu lakini akahimiza kwamba lililo muhimu zaidi ni kwa watu kupata chanjo za kwanza.