NA TATU MAKAME

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Hamid Seif Said, ameitaka jamii kushirikiana na watu wenye ulemavu katika shughuli mbali mbali ili kuweka usawa.

Akizungumza na baadhi ya watendaji kutoka jumuiya ya wakalimani wa lugha ya alama pamoja na viziwi ikiwa ni shamrashamra ya kuelekea maadhimisho ya siku ya utalii duniani, Ofisini kwake Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo, ikiwa jamii itakuwa tayari kuipa ushirikiano wa karibu kwa shughuli za kijamii, kwani wanahaki sawa na watu wengine, hivyo ipo haja kwa jamii kushirikiana nao katika harakati za maendeleo.

Akizungumzia suala la utalii Mkuu huyo amewataka wadau mbalimbali katika wilaya hiyo kuimarisha ulinzi kwa wageni wanaoingia katika maeneo yao ili kuongeza idadi ya wageni pamoja na serikali kupata mapato yake kupitia sekta hiyo.

Nae Ofisa Utalii Wilaya hiyo, Juma Mussa Juma, alisema dhana ya utalii kwa wote ina lengo la kuleta maendeleo kwa wadau wote ikiwemo wawekezaji pamoja na kutunza mazingira katika maeneo ya fukwe na kukuza utamaduni wa mzanzibari.