NA MWANDISHI WETU
MKUU wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi, amewataka wamiliki na wafanyabiashara wa vileo na maswala ya burudani kuzingatia na kufuata sheria ili kuondoa malalamiko ndani ya jamii.
Alieleza hayo juzi usiku alipofanya ziara ya kushitukiza katika baa za New Star ya Kianga, New Upepo ya Dole na Queen Masinde ya Chuini na kukuta shughuli za muziki zikiendelea bila kufuata miongozo iliyowekwa.
Alisema kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya uendeshaji wa biashara za vileo likiwemo swala la upigaji muziki kwa sauti ya juu na kusababisha kero.
“Biashara hizi (vileo na muziki) zimewekewa utaratibu hivyo lazima ufuatwe ili kuendeleza hali ya amani na utulivu ndani ya jamii,” alieleza Kunambi.
Alifafanya kuwa ili kuimarisha hali ya mani, utulivu na ustawi wa jamii, kuna haja ya kila mmoja miongoni mwa jamii kufuata sheria na taratibu.
Akiwa pamoja na maofisa kutoka baraza la sanaa, sensa, filamu na utamaduni (BASFU) na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, kunambi alitoa amri ya kusitishwa kwa shughuli za muziki katika baa hizo na kushikilia baadhi ya vifaa hadi taratibu za sheria zitakapofuatwa.
“Hatuwezi kuacha watu wachache wakakiuka sheria na kuwaudhi wengine nasi tukawatizama tuu, kuanzia sasa hakuna ruhusa ya kupigwa muziki sio katika baa hizi tuu bali maeneo yote bila ya taratibu kufuatwa,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mrajis wa Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASSFU), Juma Chum Juma, alieleza kuwa sheria ya baraza hilo inakataza upigaji wa muziki katika maeneo ya baa na kumbi za starehe bila leseni lakini pia kufuatwa kwa masharti ya leseni hizo.
Aidha Chum alimpongeza mkuu huyo wa wilaya na kamati za ulinzi na shehia za wialaya hiyo kwa ushirikiano inaoutoa kwa baraza lake ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na sheria zinazosimamia maswala ya utamaduni nchini.