NA MWAJUMA JUMA
DIWANI wa Wadi ya Dimani, Khamis Omar Khamis, amesema mazingira bora ya upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi yatawawezesha kufanya vizuri na kufaulu mitihani yao.
Hayo aliyaeleza kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi vifaa vya masomo na vyakula vyenye thamani ya shilingi 600,000, katika skuli ya Kombeni Msingi na Sekondari, Dimani na Bwefum, zilizomo katika jimbo la Dimani mkoa wa mjini Magharibi Unguja.
Hivyo alisema amemauwa kutoa msaada huo ili kuhakikisha wanafunzi hao wanakuwa mfano bora wa kufaulu masomo yao pasipo na pinmgamizi.
Wakitoa shukrani zao waalimu kutoka skuli hizo waliahidi kuvitumia na kuvitunza ipasavyo vifaa hivyo kama ambavyo vilivyokusudiwa.
Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Bwefum, Bahati Bashiru, alisema msaada huo wameupokea na umekuja wakati muafaka, kwani wanafunzi wamekuwa na mahitaji makubwa hasa katika kipindi hichi ambapo wapo kambini kujiandaa na mitihani yao.
Nae mwanafunzi Othman Ali wa skuli ya Kombeni Sekondari alisema wao kama wanafunzi wanaahidi kwamba msaada wa vifaa hivyo utakuwa ndio chachu ya wao kufanya bidii na kufaulu katika mitihani yao.
“Umetupatia msaada huu kwa moyo wako na sisi tunakuahidi tutatoa matunda mazuri katika skuli zetu”,alisema.