NA SAIDA ISSA, DODOMA
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyokamilika vianze kufanya kazi kwa kutoa huduma za afya.
Waziri huyo amebainisha hayo jijini Dodoma katika mkutano mkuu wa mwaka wa kiutendaji wa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, mkutano unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete.
“Kuna hospitali nyingi huko pembezoni zimekamilika mapungufu yapo machache anzeni kutoa huduma hata ya kuwapima watoto uzito wakina mama wanatoka mbali wanapanda gari kwaajili ya kupeleka watoto kupima tu”, alisema waziri Gwajima.
Dk. Gwajima alisema serikali imeshajenga miundombinu bora hivyo watoa huduma za afya wahakikishe wanatoa huduma bora huku akiwataka viongozi wa ngazi zote kuendelea kuhamasisha wananchi waende kupata chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 kwani huduma hiyo inapatikana katika hospitali zote hapa nchini.
Kwa upande wake, naibu waziri Tamisemi anyeshughulikia Afya, Dk. Festo Dugange aliiomba serikali juu ya utoaji wa chanjo ya Uviko 19 kuwa lazima kwa makundi yote maalumu huku akiwataka waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha miradi yote ya afya inakamilika kwa wakati.
“Fanyeni mpango miradi yote ya afya itekelezwe nawaagiza mkasimamie tuanze kuhudumia wananchi”, alisema Dugange
Kwa upande wake katibu mkuu wa wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alisema anapokea malalamiko kwamba kuna baadhi ya watumishi wa afya utendaji kazi wao hauridhishi na kuwataka waganga wakuu hao kwenda kulisimamia vyema suala hilo.
Naye katibu mkuu Tamisemi Prof. Riziki Shemdoe aliwaagizi waganga wakuu hao mambo matatu ambayo kujitokeza kwenda kuchanja, kutofikisha fedha za miradi ya maendeleo mwaka mwingine lakini pia kutambua kwamba miradi yote ya afya ni yakwao huku akiwataka wakawasimamie vyema watumishi wote wa sekta ya afya.
Awali akisoma risala akimuakilisha mwenyekiti wa waganga wakuu Dk. Japhet Simeo alisema wizara ya afya imeendelea kupita kwenye changamoto ya ungonjwa wa Uviko 19 na ni hali iliyopelekea kuwapoteza wataalamu wa afya walio wengi.