NA HAFSA GOLO

VIONGOZI wanaomsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika ngazi mbali mbali za uongozi wameshauriwa kutumia uwezo wao kuhakikisha malengo yaliyowekwa na serikali yanafikiwa.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, alipokuwa akizungumza na Masheha wa mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili, Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema ni jukumu la viongozi hao kuhakikisha juhudi za serikali ya awamu ya nane za kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanafikiwa kwa wakati uliokusudiwa.

Alisema kuchapa kazi kwa bidii na kuzingatia nidhamu na sheria za utumishi wa umma kutachangia kasi ya maendeleo na malengo kufikiwa.

“Tukifanywa hayo huku tukidumisha mashirikiano ya kiutendaji miongoni mwetu, wafanyakazi wenzetu na wananchi kwa jumla, tutakuwa tumeunga mkono juhudi za Rais wetu (Dk. Mwinyi) za kuleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba,” alieleza Dk. Khalid.

Aidha Dk. Khalid alimshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa hekima na busara zake ambazo zimechangia kuimarika kwa hali ya utulivu na amani.

“Hali hii ni kichocheo na kivutio katika utekelezaji wa azma ya Rais wetu kuiletea maendeleo Zanzibar hivyo lazima kila mmoja kwa nafasi yake adhamirie kuifanikisha,” alisema.

Dk. Khalid alisema serikali imechukua juhudi za kuhakikisha ustawi wa maisha ya wananchi yanaimarika kwa kuzingatia utawala wa sheria.

“Suala la maendeleo katika nchi yoyote duniani ikiwemo Zanzibar, linahitaji nguvu za pamoja na mashirikiano ya dhati ya kila mmoja wetu ikiwa kongozi au mwanachi,” aliongeza waziri huyo.

Alibainisha kwamba hatua hiyo iwe sambamba na watu wote wajali na kuthamini uzalendo ambao utatoa mchango katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ulinzi na usalama nchini.