NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amewataka Masheha kufichua mambo yanayosababisha uvunjifu wa sheria za nchi na kufanyika makosa ya jinai.

Aliyasema hayo wakati akizindua zoezi la utoaji elimu kwa Mashekha  katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakili Kikwajuni Mjini Unguja.

Alisema  hatua hiyo itasaidia kwa serikali kuwatambua wafanyanyaji biashara za dawa za kulevya, uddhalilishaji, wizi pamoja na wageni wanaoingia kinyume na taratibu za nchi.

Aliwataka mashekha hao kuzingatia mambo matatu ya msingi katika kusimamia majukumu yao ya kazi, ikiwemo uongozi bora, mfumo wa uendeshaji na udhibiti pamoja na nidhamu katika uwajibikaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alifahamisha kuwa endapo watafata misingi hiyo wataepuka kujihusisha na migogoro ya ardhi, vitendo vya rushwa pamoja na kushirikiana na wahalifu katika kufanya makosa.

Dk. Khalid, alitumia fursa hiyo  kupongeza juhudi za Idara ya Uhamiaji Zanzibar, kwa kuandaa zoezi hilo muhimu la kuwajengea uwezo Mashekha  pamoja na kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wageni wanaofika katika ofisi mbali mbali za Uhamiaji.

“Hii inaonesha wazi Idara yetu ya Uhamiaji inavyothamini mchango wa kila mmoja katika utoaji wa huduma hizo lakini pia katika kulinda usalama wa nchi yetu”,alisema.