NA KIJA ELIAS
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kushirikiana na Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi za Tanzania nje ya nchi, kupata teknolojia rafiki, mitaji kutafuta masoko.
Dk. Mpango aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua maonesho ya tatu ya SIDO yaliyofanyika katika uwanja wa Umoja wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Maonyesho hayo yalikuwa yamelenga kutoa fursa kwa wajasiriamali kupanua wigo wa masoko ya bidhaa, kuongeza uzalishaji, kubadilishana uzoefu, ujuzi na kuboresha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko.
Aidha, aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa malengo ya kuanzishwa kwa SIDO na kupitia mahitaji ya bajeti yake kisha kutoa mapendekezo ya mikakati mipya ya kuiboresha na kuitafuta vyanzo vingine vya mapato.
Pia alielekeza SIDO, taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha katika maendeleo na teknolojia ya viwanda zichukue hatua za dhati na kujiwekea malengo ya kulinyanyua taifa, katika utengenezaji wa mashine mbalimbali za kuchakata na kuongeza thamani mazao ya kilimo kwa kutumia teknolojia.
Makamu wa Rais, alizitaka taasisi za kifedha kubuni na kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo yenye riba nafuu kutoa elimu kuhusu ubora wa miradi usimamizi wa miradi na matumizi ya mikopo inayotolewa.
Dk. Mpango, aliliagiza Shirika hilo kuendelea kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa wananchi kuingia katika shughuli zinazotumia teknolojia rahisi na nafuu hususan katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao na bidhaa mbalimbali.
Aliitaka SIDO kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kutunisha mfuko wa taifa wa kuendeleza wajasiriamali (NEDF), na kuwapatia wajasiriamali mikopo yenye masharti nafuu, kutoa elimu, ujuzi, taarifa, mitaji kuwalea na kuwakuza.