NA HABIBA ZARALI, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa ujenzi wa majengo ya kisasa ya hospitali lazima uendane na uwepo wa vifaa kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana alipokuwa akiendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo Kisiwani Pemba wakati alipotembelea ujenzi wa hospitali ya Chakechake.

Alisema serikali itahakikisha baada ya kumalizika kwa ujenzi wa hospitali hiyo vinapatikana vifaa vya kisasa ambavyo vitawapatia huduma bora wananchi wanaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Dk. Hussein Mwinyi, alisema amefarajika kuona ujenzi wa hospitali hiyo unavyoendelea na kuahidi kutafuta fedha za ziada ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Alifahamisha kuwepo kwa ujenzi huo pamoja na vifaa utapunguza changamoto wanazozipata wananchi za kufanyiwa vipimo katika hospitali hiyo na hatimae kusomwa Unguja ama Muhimbili kwani amesikia kutokuwepo kwa mashine ya X-Ray katika hospitali hiyo.

Alieleza kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakumba watendaji wa wizara ya Afya ikiwemo stahiki zao, lakini aliwasihi kufanyakazi kwa uadilifu wakifikiria kutoa kauli mzuri kwa wagonjwa wanaofika kupatiwa matibabu.

“Nawaomba wafanyakazi wa afya muwe na kauli mzuri kwa wagonjwa kwani hiyo yote ni tiba na muelewe kuwa kazi muayoifanya ni ya wito na malipo yake makubwa mutayakuta mbele ya Mwenyezi Mungu”, alisisitiza.

Hata hivyo, aliyakubali maombi ya wananchi juu ya kuongezwa kwa majengo ya ziada baada ya wodi hiyo ya mama na mtoto linalojengwa ili wagonjwa wanaofika hapo wawe na sehemu mzuri ya makaazi.

Akizungumza suala la kupatikana chakula kwa watu wanaofika katika hospitali hiyo, alisema litaangaliwa ili kuona linafanyika kwa kuwaondolea shida wananchi hususan waliokuwa hawana jamaa.

Akitembelea mradi wa maji katika kijiji cha Chanjaani, alisema miongoni mwa vipaumbele vya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika hasa ikizingatiwa kuwa ni huduma muhimu kwa maisha ya wanaadamu.

Alieleza kuwa serikali itatafuta njia ya kuiwezesha ZAWA, kupata fedha za kusambazia mabomba ya maji kwa haraka ili tatizo walilonalo wananchi hao liweze kumalizika.