NA MWANDISHI WETU, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuna na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Lawrence Tax na kumueleza kwamba ushirikiano ndio siri ya mafanikio ya wizara hiyo.

Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo  na waziri Dk. Tax jana ikulu  Zanzibar, ambapo waziri huyo alikuja kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais Dk. Mwinyi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni  Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Mwinyi alimueleza Dk. Tax kwamba mashirikiano ya pamoja yaliopo katika wizara hiyo ndio yanayoleta mafanikio hasa mashirikiano kati ya Taasisi za Ulinzi na Wizara.

Aidha, alisema kuwa wizara hiyo ni ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameridhika kwa kazi nzuri inayofanya huku akisisitiza kwamba mashirikiano makubwa kati ya Wizara hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni makubwa.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati Dk. Tax kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kueleza kuwa ana imani kubwa kwamba Wizara hiyo iko salama kutokana na utendaji mzuri wa Waziri Dk. Tax.

Nae Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Lawrence Tax kwa upande wake alimpongeza Dk. Mwinyi kwa imani kubwa iliyooneshwa kwake na hatimae kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao aliahidi kuufanyia kazi kwa manufaa ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Dk. Tax alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo makubwa.