NA HAJI NA NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, kuangalia uwezekano wa kuwapatia uwanja wa mbadala wa mpira wa miguu, vijana wa timu za kijiji cha Mgelema wilaya ya Chake chake, kufuatia uwanja wao wa zamani, kuharibika kutoka na ujenzi wa barabara.

Alisema wizara husika inawajibu kuhakikisha ujenzi wa barabara hauathiri michezo, na hivyo ni vyema kushirikiana na wanamichezo hao, ili kutengenezewa uwanja mwengine.

Rais huyo wa Zanzibar, alitoa agizo hilo jana kijijini hapo, wakati wa ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba, katika utaratibu wake wa kupokea malalamiko na kero za wananchi kisiwani Pemba.

Alisema serikali ya awamu ya nane, ina mpango wa kuimarisha michezo mbali mbali, hivyo si busara kuona harakati za kimaendeleo, zinaathiri michezo pamoja na miundombinu yake.

Alieleza kuwa kama uwanja wa michezo wa Mgelema kwa sasa haufai kimatumizi  kutokana na kupitishwa kwa barabara iendayo kijijini hapo, ni wajibu kwa wizara husika kuhakikisha wanatengeneza uwanja mwengine.

“Niiagize wizara husika kuhakikisha wanajenga uwanja mbadala wa michezo kijijini hapa, maana ule ambao vijana wetu walikuwa wakiitumia, kwa sasa umeathiriwa na ujenzi wa barabara ya Kipapo –Mgelema hadi Wambaa, lazima wapatiwe eneo mbadala,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, alisema michezo pamoja na kwamba huzaa ajira, lakini hukimbiza magonjwa na maradhi kadhaa kwa wanaofanya mazoezi.

“Hata yule kijana ambae alikuja kulalamikia juu ya uwanja wao kuharibika kutokana na ujenzi wa barabara, tayari anaonesha kitumbo kimeanza kutoka, hivyo mazoezi yanahitajika,’’ alieleza.