NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inanufaika na msaada wa afya na vifaa unaotolewa na madaktari kutoka nchini China.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo ikulu mjini Zanzibar wakati wa kuwaaga madaktari tisa kutoka China wanaomaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar.
Alisema, China imekuwa ikitoa msaada wa kiafya hapa Zanzibar kwa kujenga miundombinu majengo, dawa, mapambano ya ugonjwa wa malaria, ujenzi wa jengo la ICU katika hospitali ya Mnazimmoja.
“Tunawashukuru kwa kutuunga mkono kwa miaka sasa misaada yetu nnayotupatia ni mengi kwani mmetuahidi kujenga hospitali ya Abdalla Mzee kwa dola milioni 14, kukabiliana na malaria na hata kulifanyia ukarabati jengo la ICU katika hospitali ya Mnazimmoja kwa dola milioni nane”, alisema.
Dk. Mwinyi, alibainisha kuwa China pia imewezesha kutoa ufadhili wa mafunzo kwa wafanyakazi mbalimbali kutoka Zanzibar kwenda kujifunza, kuongeza ujuzi na maarifa yanayosaidia kuongeza ufanisi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona pia serikali ya China ilitoa msaada wa chanjo.
Dk. Mwinyi alibainisha kuwa anaamini kwamba timu nyengine ya madaktari inayotarajiwa kuwasili leo visiwani hapa wataendelea kushirikiana na kutoa huduma nzuri za kiafya kwa wananchi.
Aliwapongeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwamba wakati wowote wanaotaka kuja Zanzibar basi milango ipo wazi.
Kwa upande wake balozi Mdogo wa China aliyekuwepo Zanzibar, Zhang Zhisheng, alisema serikali ya China itaendeleza udugu wao wa kuleta madaktari wake hapa Zanzibar kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenye matatizo mbalimbali.
Alisema uhusiano wao kati ya Zanzibar na China ulitengenezwa na Mzee Abeid Amani Karume tokea mwaka 1964 na utanaendelea kuimarika.
Alibainisha kwamba uhusiano wa Zanzibar na China wa kubadilisha madaktari umefikia miaka 54 na wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kwa serikali.
Alisema timu hiyo imefanya kazi nzuri na kuahidi madaktari wengine wanaokuja wataendelea kutoa matibabu vizuri kwa wananchi kama wengine wote waliopita na hao wanaondoka.
Naye Waziri wa Afya Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alisema alisema wafanyakazi hao walikuwa wakifanya kazi masaa 24 katika kutoa huduma kwa wagonjwa katika hospitali ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee kisiwani Pemba.
Hata hivyo alisema wataalamu hao wamefanya kazi nzuri wamewajengea ufanisi mzuri kwa madaktari wengine wa Zanzibar wa ufanyaji kazi.
Alisema anamini kwamba madaktari wapya watakaokuja kutoka chini China wataendelea kutoa hudma nzuri kwa wananchi na serikali ya china itaendelea kuunga mkono juhudi hizo za kuwasaidia madaktari kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar.
Alisema historia ya Zanzibar nz china imeanza tolea 1964 hadi sasa kwani China imeunga mkono kwenye sekta nyingi ikiwemo afya michezo kilimo viwanda.
Hivyo aliwasisitiza madaktari wa Zanzibar wayatumie maarifa na ujuzi walioupata kutoka kwa madaktari hao waliomaliza muda wa mwaka mmoja hapa nchini katika kuwapatia huduma bora za afya kwa wananchi.
Akitoa taarifa fupi ya madaktari wa China wanaofanya kazi zao Zanzibar Kiongozi Mkuu wa Madaktari wa Kichina, Dk. Wang Yiming alisema mwezi Septemba mwaka jana walikuja Zanzibar na kufanya kazi, lakini walikabiliana na changamto mbalimbali kutoka kwa wagonjwa lakini walisaidiana na madaktari wazalendo.
Walipongeza ushirikiano walioupata kutoka kwa madaktari wazalendo na kuahidi kuwa urafiki wao kati yao na Zanzibar utaendelea kudumu.
“Tungependa kubaki lakini muda wetu umemaliza na watakuja wenzetu wengine naamini mtaendelea kuwapa ushirikiano kama mliotupa sisi,” alisema.
Katika hafla hiyo Rais Mwinyi alikabidhi zawadi mbalimbali kwa madaktari hao ikiwemo medani, milango ya Zanzibar na kombe.