Awataka wakasimamie diplomasia ya uchumi

Asema wanawajibu wa kuvutia wawekezaji

NA MWANDISHI WETU, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuitekeleza sera ya diplomasia ya uchumi kwa vitendo ili kuiletea maendeleo nchini Tanzania.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Dk. Mwinyi aliwaeleza mabalozi hao kwamba sera iliyopo katika Jamhauri ya Muungano wa Tanzania ni diplomasia ya uchumi, hivyo ni vyema mabaozi hao wakaitekeleze kwa vitendo katika vituo vyao walivyopangiwa.

Alisema kuwa miongoni mwa hatua za utekelezaji wa sera hiyo ya diplomasia ya uchumi ni kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar katika sekta ya uwekezaji kutokana na fursa mbali mbali ziliopo.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar utalii ndiyo sekta iliyopewa kipaumbele kwani imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la taifa hivyo ni vyema wakaiwekea kipaumbele cha pekee.

Alieleza kuwa sekta hizo ni miongoni mwa sekta zilizowekewa mikakati maalum na serikali ya awamu ya nane katika kuimarisha uchumi wa buluu zikiwemo uvuvi, bandari, mafuta na gesi asilia ambazo zinahitaji msukumo wa viongozi hao kuzitafutia wawekezaji katika vituo vyao.

Alieleza kwamba mbali na uwekezaji bado Tanzania ikiwemo Zanzibar imekuwa ikiagiza kwa kiasi kikubwa bidhaa nje ya nchi kuliko kuzalisha wenyewe hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ya biashara ili Tanzania nayo iweze kuuza nje bidhaa zake.

Akizungumzia suala la kuimarisha amani na utulivu, Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema mashirikiano ya kuhakikisha amani na utulivu vinaimarishwa kwa pamoja hasa kwa nchi zilizopakana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Rwanda.

Alisema kuwa miongoni mwa nchi ambazo hivi sasa zimeonesha nia na kuamsha ari kubwa ya kuja kuekeza nchini ikiwemo Uturuki, ni vyema mashirikiano na uhusiano ukaimarishwa zaidi ili wawekezaji kutoka nchi hiyo wazidi kuongezeka hapa nchini.

Sambamba na hayo, alieleza haja kwa mabalozi hao kuendelea kuitangaza Tanzania hasa Marekani ambako inaonesha bado Tanzania haijatangazwa zaidi kiutalii kutokana na watalii wanaokuja kuitembelea Tanzania kuwa wachache.

Aidha aliwaeleza mabalozi hao kwamba kutayarishwa kwa kipindi cha “The Royal Tour” ambacho kimemuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuitangaza Tanzania hasa katika sekta ya utalii kutaitangaza zaidi Tanzania katika nchi za Marekani, Ulaya, Asia na Afrika.

Nao mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikishia Dk. Mwinyi kwamba watahakikisha wanatekeleza kwa vitendo Sera ya Diplomasia ya Uchumi hasa kwa kutambua kwamba hiyo ndio dira ya Tanzania hivi sasa.

Wakizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzao waliofika ikulu balozi Mahmoud Thabit Kombo na balozi Elsie Sia Kanza walimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuwapa maelekezo na kueleza matarajio waliyonayo wananchi wa Tanzania kwao katika kuyatekeleza majukumu waliyopewa.