NA HAJI NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ni wakati muafaka, hivi sasa kuwa na ligi nzuri baada ya kupatikana mfadhili.

Alisema kwa muda mrefu ligi kuu ya mpira wa miguu ilikuwa ikichezwa katika umasikini mkubwa, jambo ambalo lilikuwa linaleta shinda kwa timu kutoka Pemba kwenda Unguja kwa kukosa nauli, lakini hivi sasa hilo halitokuwepo tena.

Dk. Hussein aliyasema hayo jana uwanja wa Kinyasini wilaya ya Wete Pemba, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kisiwani humo, wakati akijibu hoja za wanamichezo juu ya utekelezaji wa ahadi zake, alizowapa wanamichezo wakati wa kampeni.

Alisema, baada ya kuingia madarakani alihakikisha ligi kuu ya Zanzibar sasa inachezwa kama ilivyo katika baadhi ya nchi, na hivyo kutafuta wafadhili ili kuhakikisha timu zinashiriki kikamilifu.

Dk. Hussein alifafanua kuwa, sasa ndani ya ligi kuu ya Zanzibar wapo wadhamini ambao wataziwezesha timu kwenda na kurudi baina ya kisiwa kimoja na chengine.

“Sasa timu za ligi kuu ya Zanzibar, kutoka kisiwa cha Pemba zitakapokwenda Unguja au za Unguja zinapokwenda Pemba, watakuwa chini ya udhamini na hapo tunachosubiri ni kukaa kwa soka letu,’’ alieleza Dk. Mwinyi.