Aipongeza IKRAAM 1 kujikita kwenye usafirishaji

NA RAJAB MKASABA

USHIRIKIANO mzuri uliopo baina ya serikali na sekta binafsi, ambao unajumuisha wawekezaji wazalendo na wageni ni suala lililopewa umuhimu na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane.

Ushirikiano huo, vile vile, umeelezwa bayana katika mipango mikuu ya maendeleo katika ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo ilielekeza serikali kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuvutia uwekezaji zaidi.

Ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi umeimarishwa kwa kutungwa na kutekelezwa kwa sheria ya mashirikiano ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public Private Partneship-PPP) ya mwaka 2015 na sheria ya baraza la biashara ya mwaka 2017.

Ni jambo la faraja sana kuona kwamba mambo yaliyobainishwa katika Ilani hiyo, yanaendelea kutekelezwa vizuri na ni vyema shukurani na pongezi za dhati zikaelekezwa kwa watendaji wa sekta binafsi wakiwemo wawekezaji wazalendo na wageni kutoka nchi mbali mbali kwa kufanyakazi kwa karibu na Serikali   katika utekelezaji wa mipango na miradi mbali mbali ya maendeleo.

Hata hivyo, ni vyema pongezi maalum zikatolewa kwa muwekezaji mzalendo, Sheikh Abdulkhafur Ismail Mohammed kwa imani, upendo na uzalendo wake kwa Zanzibar na wananchi wenzake na kwa kuwa mstari wa mbele katika uwekezaji katika usafiri wa baharini kwa kuleta meli ya abiria na mizigo iitwayo Ikraam 1, ambayo itasaidia wananchi kwa usafiri hasa wale wanaotoka upakde wa Kaskani Pemba ambao hutumia bandari ya Wete.

Sheikh Abdulkhafur Ismail Mohammed ameonesha njia na kufungua milango katika utekelezaji wa mipango ya serikali katika suala la kutekeleza uchumi wa buluu kwa kuanzisha usafiri wa baharini utakaosafirisha mizigo pamoja na abiria.

Bila ya shaka, Sheikh Abdulkhafur Ismail Mohammed na wafanyabiashara wengine wana nafasi muhimu katika historia ya maendeleo ya Zanzibar kwani mambo wanayoyafanya yatakumbukwa na vizazi vijavyo kwa miaka mingi hapo baadae.

Bila shaka serikali itaendelea na juhudi zake katika kuwawezesha na kuwaweka mazingira mazuri wawekezaji wazalendo wanaotaka kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchini kama Dk. Mwinyi alivyodhamiria katika kulitekeleza jambo hili.

Aidha, serikali itahakikisha inaongeza fursa zilizopo, ili kumuwezesha kila mwananchi kuzitumia fursa hizo vizuri kwa kutegemea uwezo wake.

Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma za usafiri zinakwenda sambamba na juhudi zinazochukuliwa na sekta binafsi katika suala hilo.

Vile vile, juhudi zilizofanywa na Serikali za kununua boti ndogo za kusafirisha abiria katika visiwa vidogo vidogo vya Unguja na Pemba ni hatua muhimu iliyolenga kuondoa changamoto mbali mbali wanazozipata wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo.

Kuwepo kwa usafiri wa baharini wa uhakika ni jambo la lazima kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote wa Zanzibar kwani ni lazima kuwepo na meli na boti za kisasa zenye uwezo mkubwa na zilizo salama kwa ajili ya kuwasafirisha abiria na mizigo yao.

Bahari ina historia kubwa katika maendeleo ya visiwa vya Zanzibar na watu wake kwani usafiri wa baharini ndio uliopelekea Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara na hatimae kuwa sehemu mashuhuri duniani kote hadi hivi sasa.

Kwa hivyo, serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi, itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na usafiri wa baharini wa uhakika, ili tuweze kufanya safari zetu za kila siku baina ya visiwa vyetu na kwenda katika sehemu mbali mbali, hasa Tanzania Bara na nchi za jirani.

Hivi sasa mataifa yote yaliyopakana na bahari, hasa nchi za visiwa, yameelekeza nguvu kubwa katika kuimarisha uchumi wa bahari (blue economy) ambao umelenga katika kufanya matumizi mazuri na bora zaidi ya bahari pamoja rasilimali zilizomo ambapo na kwa upande wa Zanzibar nayo imejikita kuelekea huko.

Ndiyo maana, mataifa kadhaa duniani, hivi sasa yameongeza kasi katika, ujenzi wa bandari za kisasa na miundombinu mingine, kuimarisha usafiri na usafirishaji, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na madini mengine ya baharini na kuitumia bahari ipasavyo katika kuimarisha biashara na utalii, na kadhalika.

Bila ya shaka, hili ni eneo muhimu kwa ajili ya uchumi wa Zanzibar, hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar imezungukwa na bahari hivyo, basi Serikali imechukua hatua ya kuandaa mikakati imara ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa kufahamu kwamba Zanzibar ina mwelekeo mzuri wa kuendeleza sekta ya mafuta na gesi, biashara na utalii sanjari na ujenzi wa bandari mpya ya mafuta na gesi asilia katika eneo la Mangapwani ambayo ni hatua muhimu katika kuendeleza uchumi wa bahari.

Kwa upande mwengine, ununuzi wa vyombo vya usafiri wa baharini unaofanywa na Serikali pamoja na wawekezaji wazalendo, vile vile, ni hatua muhimu katika kuendeleza uchumi wa bahari pamoja na sekta ya utalii, usafirishaji na biashara.

Bila ya shaka, juhudi hizi zilizofanywa na Sheikh Abdulkhafur Ismail Mohammed katika suala zima la usafiri wa baharini zina umuhimu mkubwa katika kukuza utalii na kuimarisha harakati za usafiri wa mizigo na abiria kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Hivyo basi, kwa wale wote waliobahatika kuajiriwa katika meli hii mpya na vyombo vyengine vya baharini hapa nchini ni vyema wakawa makini katika kufuata sheria na kanuni za usalama wa chombo na abiria kwani ni muhimu ikazingatiwa kwamba jambo dogo linalotokea baharini likiwa na dhara linaweza kuwa kubwa, ikiwa vyombo vya uwokozi vitachukua muda mrefu, kufika kwenye tukio na kutoa huduma.

Sambamba na hayo, ni vyema Taasisi mbali mbali zilizopo bandarini zikawa na mashirikiano mazuri kati yao na wawekezaji wote kwani wote wana lengo moja ambalo ni kuijenga nchi sanjari na kuisaidia jamii.

Kadhalika, wafanyabiashara wote na wajasiriamali ni vyema wakazingatia sheria katika kuendesha shughuli zao na wawe waadilifu hasa katika masuala ya ulipaji kodi na malipo mengine yanayotozwa na Serikali kwani uadilifu unazidisha baraka katika biashara na mambo yote yanayofanyika kila siku.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ziara yake aliyoifanya kiswani Pemba, aliizindua meli ya Ikraam 1 na kutumia fursa hiyo kumpongeza mmiliki wa Meli hiyo kwa kuitekeleza dhana ya uchumi wa buluu kwa vitendo kwa kuleta meli ambayo kituo chake kikuu kitakuwa katika Bandari ya Wete.

Katika hotuba yake Dk. Mwinyi alitoa pongezi zake kwa uongozi wa Kampuni ya meli hiyo kwa kuutekeleza uchumi wa buluu kwa kutumia fursa ya bahari iliyopo kwa ajili ya kuleta maendeleo katika jamii.

Alisema kuwa amefarajika sana kwa kuona hatua ya kuanza kwa usafiri na kumpongeza mmiliki wa meli hiyo Abdulkhafur Ismail Mohammed kwa kuisaidia Serikali katika kutoa huduma ya usafiri kwa jamii hatua ambayo itasaidia kusafirisha abiria pamoja na mizigo kutoka Wete na kwenda maeneo mengine kama vile Dar-es-Salaam, Tanga na Mombasa.

Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo ya kuleta meli kwa ajili ya usafiri wa abiria na mizigo pia, itapunguza bei ya bidhaa, kwani kuna bidhaa ambazo hutoka Mombasa, Tanga ama Dar es Salaam na kupita Unguja kwanza na ndipo zifike kisiwani Pemba hatua ambayo huzidisha bei ya bidhaa hizo kisiwani Pemba na kuleta usumbufu kwa wananchi.

Alisema kuwa safari za meli hiyo kwa wiki mara tatu kisiwani Pemba zitasaidia kwa kiasi kikubwa kwani hapo siku za nyuma kulikuwa na shida kubwa ya usafiri hasa kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini kupitia bandari ya Wete.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ikraam Juma Amour akitoa taarifa ya meli hiyo kwa niaba ya Kampuni ya Ikraam alisema kuwa Kampuni hiyo imeanzisha shughuli hizo kwa lengo la kuongeza uwekezaji wa usafiri wa baharini.

Aidha, alisema kuwa Kampuni hiyo imechagua kituo kikuu cha huduma hizo kuwa ni Wete kwa sababu za kuimarisha maisha ya wananchi wa Wete pamoja na maeneo mengine ya kisiwa hicho cha Pemba.

Kwa maelezo ya Mkurugenzi huyo, meli hiyo ya Ikraam 1, imetengenezwa mwaka 2018 nchini Ugiriki na kusajiliwa na Mamlaka ya Kimataifa ya Huduma za Baharini ambapo pia, chombo hicho kinauwezo wa kuchukua abiria 1150 na mizigo tani 400.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Kampuli ya Meli ya Ikraam 1 ina mpango wa kununua meli nyengine kwa ajili ya kupanua huduma za usafiri kwa wananchi wa Pemba hasa katika Wete ambapo pia, meli hiyo itatoa huduma zake kwa kutumia kituo chake kikuu cha bandari hiyo ya Wete kutoka Mombasa, Tanga na Dar es Saalam.

Ununuzi wa meli hiyo unakwenda sambamba na azma ya Dk. Mwinyi ya kuimarisha uchumi wa buluu huku akieleza kwamba lengo la Kampuni yao kwa hapo baadae ni kuongeza meli nyengine na kuweza kutoa ajira 300 zilizo rasmi ambapo hivi sasa tayari imeshaanza kutoa ajira 120.