NA MWANDISHI WETU, MPKR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema taifa haliwezi kusonga mbele bila ya kuwepo mipango na sera makini katika sekta ya elimu inayolenga kuwezesha na kuiongoza jamii kuelekea kwenye maendeleo.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, katika maadhimisho ya miaka 57 ya sherehe za Elimu bila Malipo, zilizofanyika Gombani.

Alisema kwamba sera hiyo imebadilishwa kwa kuzingatia mpango wa uchumi wa buluu unaolenga kupatikana wataalamu bora katika ngazi ya Vyuo Vikuu na pia kuimarisha mafunzo ya amali katika jitijhada za kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Aidha alisema hivi sasa Zanzibar inazingatia kufanya mapitio ya mitaala ya elimu ya maandalizi na msingi na kuhakikisha kwamba serikali inatatua changamoto mbali mbali zikiwemo za miundombinu na uhaba wa walimu.

Dk. Mwinyi alifahamisha kwamba jitihada hizo zinazofanywa na serikali za kuinua maendeleo ya elimu ni uwekezaji muhimu wa kimaendeleo unaodhamiria nchi kuwa na wataalamu zaidi katika sekta mbali mbali na kusaidia kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kwa jumla.

Alisema hatua kubwa iliyofikiwa katika maendeleo ya elimu Zanzibar imetokana na juhudi na ni matunda ya Mapinduzi yaliyoazimia kupatikana huduma za elimu bila malipo na kutokuwepo ubaguzi wa rangi, itikadi, dini kabila, jinsia au uwezo wa kiuchumi alionao mwananchi.

Dk. Mwinyi alisema kwamba serikali imefanikiwa kuongeza idadi ya skuli za maandalizi kufikia 312, elimu ya msingi kufikia 333 na sekondari zimefikia 218.

Alisema hatua hiyo imewezesha pia kuanzishwa taasisi za elimu ya juu kadhaa, vyuo vya ualimu na vyuo vikuu ili kutoa fursa zaidi kwa vijana wa Zanzibar kupata elimu jambo ambalo ni maendeleo makubwa ya elimu hapa Zanzibar.

Aidha alisema serikali inaendelea na juhudi za kutatua changamoto za elimu zilizopo ikiwa ni pamoja na kuongeza madarasa, vyumba na vifaa vya maabara na kuimarisha miundombinu mingine ya maendeleo ya elimu Zanzibar kwa nia ya kupata wataalamu watakaochangia kasi ya uchumi wa buluu.

Dk. Mwinyi alisema kwamba serikali pia inachukua jitihada kubwa katika kukabiliana na uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi na serikali inatoa kipaumbele katika masomo yao ili kumaliza changamoto hiyo na kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya miundombinu ya elimu inayoendelea nchini kote.

Alibainisha kuwa juhudi hizo ndio zinazosaidia kuongeza idadi ya ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya ngazi mbali mbali ikiwemo ya msingi, kidato cha pili cha nne na ufaulu wa kidato cha sita umefikia asilimia 40.5 kutoka asilimia 33.92.

Alifahamisha kwamba jitihada hizo pia zimechangia kuongezeka kwa mahitaji ya mikopo ya elimu ya juu na zaidi ya shilingi 11 bilioni zimetumika kuwapatia mikopo ya elimu ya juu jumla ya wanafunzi 4,040 wakiwemo wapya na wanaoendelea na tayari serikali imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 2.5 bilioni ikiwa ni urejeshwaji wa mikopo hiyo kutoka kwa wanufaika 2,114.

Dk. Mwinyi amewataka walimu kufanya juhudi maalum katika kuhakikisha kwamba wanarejesha hadhi ya elimu hapa Zanzibar na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na kujenga heshima ya kazi yao ya ualimu kwa kutimiza vyema malengo ya kuwafunza watoto.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohammed Said, aliwakumbusha wazazi kuendeleza haja ya kujenga mashrikiano mema katika kujenga uwezo wa watoto kupata elimu bora.

Aidha aliwataka wanafunzi kujitahidi kushughulikia masomo yao katika kuhakikisha wanajijengea uwezo na kuweza kufaulu vyema katika masomo yao kwa kujenga mustakabali wa maisha yao.

Katika risala yao iliyosomwa na mwalimu Mussa Abdulrab Fadhili waliahidi kwamba watajitahidi kushirikiana katika kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ili kutimiza malengo ya elimu bila malipo.