Zanzibar yapiga kubwa kuwapa matunzo
NA MOHAMMED SHARKSY, SUZA
MAADHIMISHO ya siku ya wazee duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na kuhamasisha jamii kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote.
Umoja wa Mataifa umetenga siku kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuimarisha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi na kuthaminiwa utu wao.
Kila mwaka, maadhimisho haya huwa yanabeba kauli mbiu yenye ujumbe mahsusi, ambapo kwa mwaka huu 2021 kaulimbiu inasema, “matumzi sahihi ya kijitali kwa ustawi wa rika zote”.
Kaulimbiu hiyo inahimiza serikali kuweka fursa sawa kwa wote bila kujali umri jinsia katika kuleta maendeleo ya sayansi na teknolojia za kileo duniani kote jamii na wadau wengine kutafakari na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, mauaji, ubaguzi na dhuluma dhidi ya wazee vitendo ambayo ni kinyume dhidi ya haki za binadamu.
Katika kipindi hichi cha maadhimisho hatuna budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia, jamii, watu wenye hekima na walezi katika jamii.
Hivyo jamii inaowajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua pale ambapo mzee ananyanyaswa au kutendewa isivyostahili.
Kwa hapa Zanzibar maadhimisho haya yatafanyika katika kijiji cha Kitope wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah na katika maadhimisho hayo kutakuwa na utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa COVID 19 bure kwa wazee wote watakaohudhuria.
Uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufika uzee. Hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla mtu huwa anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pakazi au katika ukoo.
Wazee tulionao aidha walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri au ni wale walioko vijijini ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi.
Katika nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa kustaafu ambao ni miaka 65. Pamoja na ukweli kwamba watumishi walio katika serikali na taasisi zake wanastaafu wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale waliojiajiri wanakoma kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweli unabaki kwamba binadamu mwenye umri wa miaka 60 anaonyesha dalili 2 dhahiri za kuishiwa nguvu.
Sera ya Taifa ya Afya na sheria ya utumishi wa umma zinazingatia umri wa miaka 60 kuwa ni kigezo cha uzee. Kwa madhumuni ya sera hii, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 na kuendelea.
Uzee na kuzeeka ni suwala lenye umuhimu mkubwa kwa jumuiya ya kimataifa hasa kuhusiana na mitazamo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Taarifa za umoja wa mataifa (1999) zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wazee duniani.
Ongezeko hili linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo kuwahudumia katika nyanja za afya, lishe na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.
Kulingana na taarifa hizo, mwaka 1950, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwepo kwa watu milioni 200 wenye umri wa miaka 60 na zaidi. Mwaka 1975, idadi hiyo iliongezeka na kufikia millioni 350. Idadi hiyo ilitegemewa kuongezeka na kufikia milioni 625 ilipofika mwaka 2005.
Pia inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2050, idadi ya wazee, kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu, itaongezeka na kuzidi ile ya watoto/vijana chini ya miaka 24.
Idadi hiyo katika bara la Afrika pekee inategemewa kuongezeka kutoka milioni 38 ya sasa na kufikia milioni 212 ifikapo mwaka 2050. Kuongezeka kwa idadi na asilimia ya watu ni mafanikio kwa kuwa ni kielelezo cha ubora wa maisha unaotokana na kuboreka kwa huduma kama vile za afya na elimu.
Hata hivyo ongezeko hilo ni changamoto kwa sababu serikali inawajibika kuwa na miundombinu inayohusika kutoa huduma kwa wazee. Hii ni nafasi muafaka kwa jamii kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Wazee wengi huishi katika umaskini hali ambayo inaleta mashaka makubwa kwao.
Kadhalika ukweli ni kwamba idadi kubwa ya wazee (takribani asilimia 75) wanaishi vijijini na kwamba idadi ya wazee wanawake ni kubwa zaidi kuliko wazee wanaume unaleta changamoto ya ziada.
Upo umuhimu mkubwa kwa serikali, taasisi zake na wakala za hiari kuandaa mazingira yanayowatambua wazee na yanayotoa nafasi kwao kushiriki kwa ukamilifu katika maisha ya kila siku ya jamii.
Serikali inatambua kwamba wazee ni rasilimali na hazina kubwa katika maendeleo ya nchi yetu. Kuwapo kwa taifa la Tanzania ni kielelezo tosha cha mchango mkubwa wa wazee walioutoa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.
Kuelekea siku hii ya wazee duniani kuna haja kubwa sana ya kuwashughulikia wazee wetu kutokana na jitihada kubwa walizitotufanyia wakati tuko wadogo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina Mipango na mikakati mizuri ya kuwatunza wazee kwa kuwajengea nyumba maalum za kuishi sambamba na kuwapatia matunzo kwenye mkaazi hayo yaliyopo Unguja na Pemba.
Aidha kwa kutambua ugumu wa maisha wanaopitia wazee Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawapatia pencheni ya shilingi 20,000 kila mwezi wazee waliofikia umri wa miaka 70.
Kwa kuzingatia hayo wazee wanamahitaji makubwa na kuzeeka au kuwa mkongwe hakuondowi utu na haki za msingi za mwanadamu, kama inavyosema ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya kuadhimisha siku hii ya Kimataifa ya wazee duniani.
Miaka 40 tangu kutangazwa kwa azimio la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1991.
Umoja huo ulianzisha siku hii ya kuwaadhimisha wazee, kwa lengo la kutoa ulinzi kwenye masuala ya uhuru, ushiriki, huduma, heshima na utu wao. Umoja wa Mataifa unasema ni jukumu la vizazi vyote kulinda haki ya jamii inayozeeka.
Kila mkongwe anahitaji heshima na kutambuliwa katika mchango wake za kuchagia kupatikana kwa mabadiliko kwa vizazi vyao.
Kila mmoja wa wazee hawa anahitaji heshima na kutambuliwa nakuthanminiwa utu wake katika mchango wake na juhudi zake za kuchagia kupatikana kwa mabadiliko kwa vizazi vyao.
Pamoja na ukweli huo huduma za afya hazipatikani kwa urahisi kwa wazee walio wengi na mara nyingi huduma hizo ni ghali. Watumishi wa afya wanaohudumia wazee hawaonyeshi mwamko na hawana mafunzo ya kutosha katika eneo hili la huduma.
Wanawake wazee na mila zilizopitwa na wakati. Wanawake wazee huathirika zaidi na matatizo ya uzee. Wanawake huishi kwa muda mrefu zaidi kuliko wanaume.
Isitoshe wanawake wazee hupambana na matatizo yanayohusiana na jinsi yao. Wazee wanawake hukosa haki ya kurithi na kumiliki mali ikiwa ni pamoja na ardhi.
Kwa baadhi ya maeneo wanawake wazee wamekuwa wakilaumiwa kubakwa na kuuawa kwa imani za uchawi. Wanawake wazee wenye ulemavu. wamekuwa hawapati fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali yanayohusu maendeleo na ustawi wao.
Wakati wanawake wamekuwa wanabaguliwa kutokana na jinsi yao, watu wenye ulemavu hawapati fursa ya kushiriki katika kujiletea maendeleo kutokana na hali zao.
Kadhalika wazee wamekuwa hawatambuliwi ipasavyo hali ambayo inasababisha kutopata haki wanayostahili kama kumiliki na kurithi mali, isitoshe wazee hao hudhuriwa kutokana na mila potofu.
Kutokana na kukosa ulinzi wa kisheria, Wazee wanadhulumiwa mali zao, hawapati matunzo wanayostahili, wazee wanawake wanakosa haki ya kumiliki na kurithi mali wanapofiwa na waume zao. Mfumo wa maisha ya kijamii hautoi nafasi ya ulinzi na usalama kwa wazee kama kundi maalum. Sababu za kuwa na Sera ya Wazee.
Kutokana na hali na mazingira ya wazee, upo umuhimu wa kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee itakayokuwa mwongozo katika utoaji huduma na ushiriki wa wazee katika maisha ya kila siku.